Watu 34 wameripotiwa kuuawa na wengine 29 kujeruhiwa kufuatia shambulio katika mnada wa ng'ombe mjni Postiskum, Kaskazini mwa Nigeria.
Utawala wa nchi hiyo umesema kuwa shambulio hilo lilikuwa ni la kulipiza kisasi kwa mauaji ya mtu mmoja yaliyofanywa na wafanyabiashara waliomtuhumu kutaka kuiba ngombe katika soko hilo.
Mtu mmoja ambaye alikuwa katika soko hilo wakati wa uvamizi huo, ameiambia BBC kuwa watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki, washambulia soko hilo jana usiku wakitumia mabomu huku wakiteketeza vibanda vilivyojengwa.
Milio ya milipuko na moto huo ulisababisha hali ya wasi wasi miongoni mwa wachuuzi katika soko hilo, ambao walianza kutoroka kutoka eneo hilo.
Wavamizi hao waliziba milango yote ya soko hilo na kuwafyatulia risasi wale waliokuwa wakitoroka.
Msemaji wa kikosi maalum ya jeshi ambalo limetumwa katika eneo hilo, amesema wanashuku wapiganaji wa Kiislamu wa Boko Haram.
Kanali Dahiru Abdussalam, amethibitisha kuuawa kwa watu 34, lakini baadhi ya wafanya biashara wanasema huenda idadi hiyo ikaongezeka na kufikia watu 50.
Serikali ya nchi hiyo imekanusha madai kuwa, jeshi lilifahamishwa kuhusu tishio la kutokea kwa shambulio hilo na halikufanya lolote kuzuia ili kuokoa maisha.
0 Comments