WARSAW, Poland
MSHAMBULIAJI wa Ureno, Cristiano Ronaldo jana alifufuka na kuipandisha ndege Uholanzi kurejea kwao baada ya kuiongoza timu yake ya taifa kushinda kwa mabao 2-1 katika mechi ya mwsiho ya kundi B kwenye michuano ya Euro 2012.
Kutokana na matokeo hayo, Uholanzi ambayo ilikuwa inapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo imeondolewa ikiwa haina pointi hata moja.
Ronaldo ambaye hakufanikiwa kuonyesha kiwango kizuri kwenye michezo miwili ya awali dhidi ya Denmark na Ujerumani, alianza kwa kuisawazishia Ureno katika dakika ya 27, akifuta bao la dakika ya 11 lililofungwa na Rafael Van De Vaart.
Mshambuliaji huyo wa Real Madrid alipambana zaidi na kufunga bao safi katika dakika ya 74 ya mchezo baada ya kuwapiga chenga mabeki wawili wa Uholanzi.
Katika mchezo mwingine, Ujerumani ilifanikiwa kuiangamiza Denmark na kumaliza kundi hilo bila kufungwa, shukrani kwa mabao yaliyofungwa na Lukas Podolski katika dakika ya 19 na Lars Bender.
Denmark ilijipatia bao lake kupitia kwa Michael Krohn-Dehli. Ujerumani na Ureno ndiyo zimefanikiwa kuingia kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa Bara la Ulaya.
0 Comments