Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Mbrazili Marcio Maximo.
Na Khatimu Naheka
KOCHA wa zamani wa Taifa Stars, Mbrazili Marcio Maximo, jana alishindwa kutua nchini baada ya majadiliano kati ya Yanga na timu yake kushindwa kufikia mwisho.
Awali ilitangazwa kuwa Maximo ambaye sasa anaifundisha Democrata ya nchini kwao angetua nchini jana, lakini taarifa zinasema kuwa kocha huyo ameshindwa kutua kwa kuwa kuna mazungumzo kati ya Yanga na timu hiyo hayajakamilika.
Mmoja kati ya viongozi wa Yanga ambaye anashughulikia ujio wa kocha huyo ameliambia Championi Jumatatu kuwa imeshindikana kwa kocha huyo kutua nchini kwa kuwa kuna mazungumzo kati ya klabu yake na Yanga yanaendelea.
“Unajua awali ilikuwa aje katikati ya wiki iliyopita ikashindikana na kusogezwa mbele mpaka leo (jana), lakini bado kuna tatizo kwani bado pande hizi tatu yaani klabu yake, Maximo mwenyewe na uongozi wa timu yetu hawajaweza kukamilisha mazungumzo,” kilisema chanzo hicho huku kikiendelea kusema:
“Nadhani sasa ndiyo unaona hata viongozi wanashindwa kusema atakuja lini kutokana na kikwazo hicho, lakini wakati wowote chochote kinaweza kutokea hasa katika wiki ijayo (wiki hii).”