Davies Mwape |
UWEZEKANO wa mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Davies Mwape, kuendelea kuichezea timu hiyo ni mdogo baada ya hivi karibuni kutamka kuwa anatakiwa na klabu mbili nchini Afrika Kusini.
Mshambuliaji huyo raia wa Zambia, wiki iliyopita alitua nchini akitokea kwao ambapo anakamilisha taratibu za kuihama klabu hiyo kwa kuwa ameonekana hana msaada mkubwa kikosini.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mwape alisema klabu mbili za Afrika Kusini zinamhitaji kwa ajili ya kwenda kuzichezea katika msimu ujao wa ligi kuu ya nchini humo.
Mwape alisema wakala wake ambaye hakutaka kumtaja jina, ndiye anashughulikia usajili wake lakini Mzambia huyo aliyeifungia Yanga mabao sita msimu uliopita, amesita kuzitaja timu hizo akidai atafanya hivyo baada ya taratibu za uhamisho kukamilika.
Mkataba wa mshambuliaji huyo aliyetua Yanga kwa makeke Juni 2010, lakini akashindwa kufanya kile kilichotarajiwa na mashabiki, unatarajiwa kumalizika Oktoba, mwaka huu.
“Klabu mbili za Afrika Kusini zimeonyesha nia ya kunisajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, lakini kabla ya kusajiliwa nitaenda huko kufanya majaribio.
“Kuzitaja timu hizo kwa sasa siwezi, kwani bado ni mapema, baada ya kumalizana kila kitu nitaziweka wazi, wakala wangu bado anaendelea kufanya mazungumzo,” alisema Mwape.
Mwape aliiwezesha Yanga kutwaa taji la ubingwa msimu wa 2010/11 na ubingwa wa Kombe la Kagame 2011.
0 Comments