Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa kazi za Tume hiyo jana(Jumanne, Juni 19, 2012) katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam. Kulia kwa Jaji Warioba ni Dkt. Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Tume hiyo na kushoto ni Bw. Assaa Rashid, Katibu wa Tume.
Baadhi ya Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakifuatilia maelezo ya Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Joseph Warioba wakati akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa kazi za Tume hiyo jana (Jumanne, Juni 19, 2012) katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia maelezo ya Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Joseph Warioba wakati akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa kazi za Tume hiyo jana(Jumanne, Juni 19, 2012) katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatarajia kuanza awamu ya kwanza ya kazi ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya katika mikoa nane itakayofanywa na makundi saba ya Tume hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana (Juni 19, 2012) jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Joseph S. Warioba ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga.
Jaji Warioba, alisema kuwa kila kundi litafanya kazi katika mkoa mmoja kwa wastani wa mwezi mmoja isipokuwa kwenye mikoa iliyo midogo kwa eneo, ambapo Tume itatumia muda mfupi.
Pamoja na kuitaja mikoa hiyo, Jaji Warioba pia aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kushiriki kazi kutoa maoni kwa uhuru na uwazi.
“Tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi na kutoa maoni yao kwa uhuru, uwazi, bila ya hofu yoyote na kwa utulivu. Tunaomba wananchi wawe wavumilivu na watoe maoni bila jazba au kubeza. Tunaomba wananchi wawe wavumilivu sana kusikiliza mawazo ya wengine hata kama hawakubaliani na mawazo hayo, “ alisema Jaji Warioba katika mkutano huo uliohudhuriwa na Wajumbe wengine wote wa Tume hiyo.
Katika mkutano huo, Jaji Warioba waliwaambia waandishi wa habari kuwa Tume imeanzisha tovuti (www.katiba.go.tz) ili kuwawezesha wananchi hususan walio nje ya mipaka ya Tanzania kupata taarifa za Tume hiyo na kushiriki katika kutoa maoni.
Pamoja na tovuti, Mwenyekiti huyo pia alisema Tume hiyo itatumia mitandao ya kijamii ya kisasa kama twitter, facebook na blogu katika kukusanya maoni.
“Pamoja na mikutano mbali mbali itakayofanyika katika mikoa yote, tutakuwa na mfumo wa kupokea maoni ya Watanzania wa kutoka pande zote za ndani ya nchi na nje ya nchi kupitia simu, barua pepe, mitandao ya kijamii kama facebook, twitter na blogu na tovuti na pia kwa njia ya posta,” alisema.
leo, (Jumatano Juni 20, 2012), Mwenyekiti huyo atafanya mkutano na waandishi wa habari wa Zanzibar mjini Zanzibar na kesho (Alhamisi, Juni 21, 2012) atakutana na Wakuu wa Mikoa na Wilaya wa Zanzibar