Na. Luppy Kung’alo, Dodoma
DODOMA JUMANNE JUNI 12, 2012.
Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma linawasaka Watu wawili kwa tuhuma za Unyang’anyi wa kutumia nguvu baada ya kuwatisha kwa jambia wasichana wawili raia wa Uholanzi na kisha kuwapora vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni moja laki mbili na sitini na nne elfu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Bw. ZELOTHE STEPHEN alisema Tukio hilo lilitokea muda wa saa saba na dakika arobaini na tano mchana katika eneo la area D Wilaya ya Dodoma Mjini, Karibu na nyumba inayojengwa kwa ajili ya 0fisi na Makazi ya Mh. Waziri Mkuu Bw. MIZENGO KAYANDA PETER PINDA.
Alitaja vitu vilivyoporwa katiika tukio hilo kuwa ni Kamera ya digitali aina ya Canon, Simu mbili za mkononi aina ya Nokia na Samsung, Begi la Mgongoni, Viatu vya wazi pea mbili (Sandal) Taulo la Hostel, Sketi, Wallet na Pesa za kitanzania shilingi 40,000/=.
Aidha aliwataja Waathirika wa Unyang’anyi huo kuwa ni wa LISA D/O LEMEN mwenye umri wa miaka (19) na FLEUR D/O EDITH SCHOLTEN Mwenye Umri wa miaka (17) wote ni Raia wa Uholanzi ambao wako nchini kama waalimu wa shule ya msingi na sekondari ya Saint Germa iliyoko jijini Arusha inayofundisha watoto ambao wazazi wao wamefungwa gerezani.
“Raia hao wa Uholanzi ambao walikuja kutembea Mjini Dodoma wakitokea Arusha walifikia katika Hostel ya Saint Maria ambayo wanaishi wanafunzi wa kike wanaosoma katika shule za kutwa za mjini Dodoma”:
Kamanda ZELOTHE STEPHEN alisema kuwa wageni hao walioporwa vitu hivyo, baada ya kufika katika eneo hilo wakiwa na mwenyeji wao aliyejulikana kwa jina la Sister PONSIAN PROTAS MATAKA miaka (43) ambaye anaishi katika Hostel waliyofikia wageni hao ya Saint Maria ilyopo eneo la Uhindini.
Alisema walipofika katika eneo hilo ambalo lina mlima kwa lengo la kupiga picha walimkuta mlinzi wa eneo hilo na Sister PONSIAN akamuuliza mlinzi kuhusu usalama wa eneo hilo akajibiwa shwari ndipo akawaacha wageni wake hao waendelee na shuguli iliyowapeleka hapo.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Bw. ZELOTHE STEPHEN alisema wakiwa katika shughuli zao, walitokea vijana wawili wasio wafahamu wakiwa na Jambia na kuwataka kutoa kila kitu walichokuwa nacho, na ndipo mmoja wa watuhumiwa akawasachi na kupora vitu hivyo kisha kutokomea kusikojulikana.
Kamanda huyo wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dododma alisema kwamba jeshi lake limeanzisha msako mkali kuhusiana na tukio hilo na pia kutoa wito kwa waananchi wanaoishi karibu na eneo husika pamoja na wananchi wote kwa ujumla, kwa kupitia mkakati wa Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi kushirikiana kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kwa pamoja kuweza kuzuia vitendo vya uhalifu katika maeneo yao.
Wakati huo huo jeshi la Polisi mkoani Dodoma linawashikilia watuhumiwa thelathini na nane kwa makosa mbalimbali ya uhalifu ikiwemo Pombe ya Moshi Lita (38), Mitambo mi nne ya kutengenezea gongo, Vipodozi mbalimbali Vilivyopigwa marufuku kwa matumizi ya binadamu pamojana misokoto Mitano ya Bhangi katika yilaya ya Dodoma Mjini.
0 Comments