Na Mwandishi Wetu
SIKU chache baada ya kutua nchini, Kocha Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic, raia wa Serbia, ameibuka na kusema yupo tayari kucheza dhidi ya Yanga mechi yoyote ile, hata kama itakuwa ni ya kirafiki.
Mara ya mwisho, Milovan aliiongoza Simba kuichapa Yanga kwa mabao 5-0 katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Jana, Milovan ameliambia Championi Ijumaa kuwa kama muda unaruhusu, yupo tayari kucheza dhidi ya Yanga katika mechi ya kirafiki na unaweza kuwa mchezo wa kuviweka sawa vikosi vyao.
Kocha huyo ametaja sababu tatu zinazomfanya ajiamini ambazo ni kuiona Yanga ni timu kama nyingine, kikosi chake kuwa na wachezaji wengi wapya lakini pia mechi ya mwisho alicheza dhidi ya timu hiyo na anajua afanye nini kuikamata.
Championi: Huoni kama hiyo ni mechi kubwa haipaswi kuwa ya kirafiki?
Milovan: Ukubwa wake ni nini? Hizi ni timu na zinaweza kujiandaa kwa michezo migumu.
Championi: Ukifungwa sasa utawachanganya wachezaji wako kisaikolojia?
Milovan: Si kweli, Yanga ni timu ya kawaida, ndiyo tumeifunga mabao matano na hatukufanya hivyo kwa JKT.
Championi: Unataka ucheze nao lini?
Milovan: Hata kesho, ila sasa ratiba kama imebana, tuna mechi za kirafiki halafu tutaweka kambi Zanzibar na siku chache baadaye ni Kombe la Kagame.
Championi: Unakiamini sana kikosi chako?
Milovan: Lazima nifanye hivyo, wale ni sawa na wanajeshi wangu na ninalazimika kuwaamini na kushirikiana nao.
Championi: Umekionaje kikosi kipya?
Milovan: Sijaanza kazi ya kufundisha, ila kuna vitu ninajipanga. Itakuwa timu nzuri, wachezaji wageni pia wamenivutia ila ninahitaji muda kukaa nao na kujua mengi zaidi kuhusu wao.
Yanga nayo imekuwa ikiendelea na mazoezi chini ya Kocha Msaidizi, Fred Felix Minziro huku ikiwa imesheheni wachezaji nyota kibao ambao Milovan ameonyesha kutokuwa na hofu nao hata kidogo.