Polisi nchini Kenya wamesema kuwa wafanyikazi sita wa shirika la kutoa misaada
kwa wakimbizi wametekwa nyara katika kambi ya wakimbizi ya Ifo ilioko kaskazini
mashariki mwa nchi hiyo.Waliotekwa ni wafanyikazi wa shirika la Norwegian Refugee Council, ambalo
linatoa huduma kwa wakimbizi kutoka Somalia wanaoishi kwenye kambi hiyo.
Msemaji wa Shirika hilo, amedhibitisha tukio hilo na kuongeza kuwa katibu
mkuu Elizabeth Rasmussen alikuwemo kwenye msafara uliovamiwa lakini
amenusurika.
Hata hivyo shirika hilo halijatoa taarifa zaidi kuhusu tukio hilo na watu
waliotekwa.
Mkuu wa wilaya ya Lagdera ambako kambi hiyo ipo Robert Kimanthi amesema
waliotekwa ni raia wa Canada, Norway, Mfilipino, Mpakistani na Wakenya wawili.
Wote ni wanaume.
Kulingana na polisi watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki walishambulia
msafara wa magari katika kambi hiyo ambayo inatoa makaazi kwa zaidi ya wakimbizi
nusu milioni kutoka Somalia. Mtu mmoja aliuawa kwenye tukio hilo.
Polisi wanashuku kuwa wapiganaji wa kiisalamu wa Al shaabab walihusika na
shambulio hilo.
Visa vya mashambulio ya kigaidi vimeongezeka katika maeneo ya kaskazini mwa
Kenya, baada ya wanajeshi wake kuingia nchini Somalia mwaka jana kupambana na
wanamgambo wa al shabaab.
Katika miezi ya hivi karibuni, wafanyakazi kadhaa wa mashirika ya kutoa
misaada wametekwa nyara katika kambi hiyo ya Daadab.
Wawili kati yao ni wanawake wawili raia wa uhispania ambao walitekwa nyara
mwezi Oktoba mwaka uliopita.
0 Comments