BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limemsimamisha kazi Mkuu wa Idara ya Utafiti, Tathmini na Huduma za Kompyuta wa Baraza hilo, Joseph Mbowe kutokana na kubainika dosari kwenye matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2012 kwenye somo la dioni ya kiislamu (Islamic Knowledge).
Katika hatua nyingine, baadhi ya Waislamu jana walikusanyika na kufanya mkutano katika viwanja vya Kidongo Chekundu, Mnazi Mmoja, Dar es Salaam wakiitaka Serikali shinikize viongozi wa juu wa NECTA akiwamo Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Joyce Ndalichako wajiuzulu, kutokana na dosari hizo.
Kusimamishwa kazi kwa Mbowe, kulielezwa katika taarifa iliyotolewa na NECTA ikiwa imesainiwa na Dk. Ndalichako na kutumwa kwa vyombo vya habari, kuwa Mkuu huyo wa Idara alisimamishwa kazi kuanzia jana.
“Kutokana na kasoro zilizojitokeza kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2012 ya somo la Islamic Knowledge na kwa kuzingatia uamuzi wa Serikali wa kuunda Kamati ya Uchunguzi kufuatilia chanzo cha dosari hiyo, Baraza la Mitihani Tanzania limemsimamisha kazi Joseph Mbowe, Mkuu wa Idara ya Utafiti, Tathimini na Huduma za Kompyuta kuanzia Juni 08, 2012.

“Uamuzi huu unafanyika ili kutoa fursa kwa Kamati itakayoundwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iweze kufanya uchunguzi wa chanzo cha dosari iliyojitokeza,” ilisema taarifa hiyo.
Waislamu waliokusanyika Kidongo Chekundu, waliitaka Serikali kuwashinikiza kujiuzulu viongozi hao kwa kile walichodai kuwa ni hujuma wanayoifanya dhidi ya wanafunzi wa kiislamu.
Kiongozi wa Waislamu hao, Kondo Juma alisema wametoa siku saba kwa Serikali kuwalazimisha viongozi hao wajiuzulu na baadaye iundwe Kamati itakayochunguza mwenendo wa usahihishaji wa mitihani ya Islamic Knowledge katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, ili kuangalia usahihi wa alama walizopewa wanafunzi Waislamu.
Juma alisema ujumbe wa Waislamu ulikutana jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, na kuwasilisha matakwa yao ya kutaka viongozi hao wa NECTA wajiuzulu mara moja.
“Kwa vile hatukumkuta Waziri (Dk. Shukuru Kawambwa) tulimwachia ujumbe wetu Katibu Mkuu na kumwambia tunahitaji majibu ndani ya siku saba na baada ya hapo, kama hatutajibiwa, tutafanya maandamano na mkutano mkubwa kuliko wa leo. “Tunachokitaka ni kwanza viongozi hao wajizulu ndipo iundwe Tume ya kuchunguza matokeo ya mitihani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita ili tuweze kujiridhisha. Tunataka wajiuzulu kwanza kabla ya kuundwa Tume ili uchunguzi huo uwe huru,” alisema Juma.
Akizungumza juzi na waandishi wa habari Dar es Salaam, Waziri Kawambwa alisema tume hiyo itaundwa na wajumbe kutoka Idara ya Ukaguzi wa Elimu, Idara ya Elimu ya Sekondari, Jopo la Wataalamu wa kiislamu linaloandaa mitaala, Baraza la Wakuu wa Shule za Kiislamu, Necta na wengine watakaoonekana wanafaa.
Kiini cha tatizo hilo ni mfumo wa kuonesha uchakataji uliotumika kutioa matokeo ulipiga hesabu za wastani wa mitihabni mitatu badala ya miwili.
Hivyo alisema tofauti za alama iliyobainika ilitokana na mfumo wa ukokotoaji kwa njia ya kompyuta kuendelea kutumia mitihani mitatu katika kupata wastani wa alama.
                                                  HABARI LEO JUNE 09, 2012