Ataka umiliki ardhi uendelee kuwa chini ya serikali
-Asema wanapiga hilo ni mabepari
NA BASHIR NKOROMO, NJOMBE
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kusiistiza juu ya msimamo wake wa ardhi kuendeleakumilikiwa na serikali kwa maslahi ya taifa zima.
Msimamo huo ulielezwa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye (Pichani) alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Turbo mjini Njombe.
Nape alisema, tofauti na mapendekezo ya baadhi ya vyama vya siasa kwamba ardhi imilikiwe na wananchi, CCM inaona kwamba bado kuna ulazima wa ardhi kuwa chini ya miliki ya Serikali, kwa sababu kuwafanya hivyo kuna faida kubwa zaidi.
“Sisi Chama Cha Mapinduzi, baada ya kutafakari kwa kina, katika rasimu yetu kuhusu katiba mpya ya Tanzania tumependekeza pamoja na mambo mengine, kwamba ardhi iendelee kumilikiwa na serikali kwa sababu tunaona kwamba utaratibu huu ndiyo unaifanya ardhi kuwa mali ya wanancho wote”, alisema Nape.
Alisema, madhara ya ardhi kumilikiwa na watu binafsi katika nchi ni jambo la hatari sana, kwa sababu inaweza kumilikiwa na mabepari wachache hata wasiozidi wanne nchi nzima kama ilivyo katika baadhi ya nchi jirani hatua inayowafanya raia kulazimika kuwapigia magoti mapepari wanapohitaji hata eneo dogo tu kufanyia shughuli zao.
Nape aliwataka Watanzania kuunga mkono hoja ya CCM ya kuendelea kuifanya ardhi kuwa chini ya miliki ya watu binafsi na kuachana na ile ya Chadema inayosisitiza kutaka ardhi imilikiwe na watu binafsi.
“Hawa Chadema wanatetea umiliki wa ardhi kuwa chini ya watu binafsi kwa sababu wana maslahi nalo, maana tunajua mwanzilishi wa chama chao ni mmoja wa matajiri wanaomiliki ardhi kubwa sana hapa nchini, sasa wanapendekeza hivyo ili mwanzilishi huyo wa chama chao asije akapokwa eneo hilo baada ya katiba mpya kutoa maelekezo kwamba ardhi ni mali ya umma kupitia umiliki wa serikali”, alisema.
Katika hatua nyingine, Nape amewataka watendaji wa mkoa mpya wa Njombe wanaohusika na upimaji viwanja, kuhakikisha wanafanya kazi hiyokwa kuzingatia haki ili kusitokee malalamiko kwa yeyote kunyimwa eneo kwa hila yoyote.
Nape alisema, kupima vbiwanja kwa kuzingatia haki kutawezesha kila mwananchi kupata eneo analohitaji kulingana na sheria, lakini isipozingatiwa hivyo, wanyonge hawatapa ardhi kwa kuwa haki isipozingatiwa ni matajiri tu ndio watakaopata maeneo tena makubwa sana.
“Mimi kama msemaji wa Chama Cha Mapinduzi kilichiunda serikali iliyopo madarakani, nawaagiza viongozi wa mkoa huu mpya tangu wa serikali na wa CCM ngazi zote, kuwa makini na hili kwa sababu ardhi ni miongoni mwa mambo ambayo huzusha sana migogoro jambo ambalo hatutaki kabisa litokee hapa”, alisema.
Akizungumzia uhai wa Chama Cha Mapinduzi, Nape alisema, CCM bado ni imara kutokana nna misingi yake, na itanedelea kutawala tangu jana, leo na kesho kwa sababu ya misingi hiyo, hivyo wana-CCM waendelee kutembea kifua mbele.
Nape aliwataka wana CCM nchini kote, kupuuza propaganda za baadhi ya vyama vya siasa za kujaribu kuonyesha kwamba CCM imechoka kuwatumikia wananchi.
“Si kweli kwamba CCM imechoka, bado ni imara na ndiyo maana kila mara tumekuwa tukifanya mageuzi kuhakikisha kinaenda na wakati, na kutokana na mageuzi tuliyomo sasa nawahakikishieni kwamba baada ya uchaguzi ndani ya chama mwaka huu, CCM itakuwa chama bora zaidi kuliko chama chochote cha siasa Tanzania na duniani kote”, alisema na kuongeza;
“Katika uchaguzi huo, CCM itahakikisha mafisadi na wala rushwa na wasio na uzalendo kwa nchi hii, hawapenyi na kujiingiza katika uongozi, kwa sababu atakayebainika kujaribu kutumia rushwa kujipenyeza ili apate uongozi wakati si msafi na hana sifa tunazotaka tutamshughulikia kwa nguvu zote.
Aliwataka wana CCM kuhakikisha fursa ya uchaguzi ndani ya Chama unaofanyika mwaka huu, kuitumia vizuri ili kukifanya chama kiwe imara zaidi kwa manufaa ya taifa akinukuu kali ya hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwamba “Bila CCM Makini Nchiye Itayumba’.