Mpango wa serikali wa kuhakikisha watu wanaoishi mabondeni wanaondolewa kwa nguvu umeanza kutekelezwa na sasa nyumba 217 za wakazi wa eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam zitabomolewa wakati wowote kuanzia sasa.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Gaudence Nyamwihura, jana aliwaeleza wabunge wa Kamati ya Hesabu za Serikali kuwa kiasi cha Sh. milioni 41 zimekwisha kupatikana kwa ajili ya gharama za kutekeleza zoezi hilo haraka.

Nyamwihura alisema nyumba hizo zitakazobomolewa ni za kuanzia eneo la bonde hilo linapokutana na habari (Delta) hadi Ananasifu na Jangwani na kwamba mkakati huo utakuwa endelevu kwa kuhakikisha watu wanaacha tabia ya kujenga mabondeni na kusababisha serikali kuingia gharama kwa kuwahamisha yanapotokea mafuriko.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Paniel Lyimo, alisema watu waliojenga mabondeni nyumba zao zitabomolewa na hawatalipwa fidia kwani maeneo kama Jangwani ni ya mkondo wa maji, lakini bado watu wamejenga nyumba kinyume cha sheria.

Lyimo alisema kuwa pamoja na mkakati wa serikali wa kutaka kuhakikisha watu hawajengi makazi mabondeni, lakini bado kasi ya halmashauri tatu za Mkoa wa Dar es Salaam imekuwa ndogo kutokana na mahitaji ya viwanja.



Alisema wananchi wanaohamishwa mabondeni ni lazima wapewe viwanja katika maeneo mengine.

Lyimo alisema hata hivyo, serikali inaendelea kuwatambua wataaalam waliohusika kutoa vibali vya ujenzi kwa wananchi waliojenga mabondeni ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Alisema utekelezaji wa mkakati wa kuwaondoa watu waliojenga mabondeni wakati mwingine umekuwa ukikwamishwa na wananchi wenyewe ambao wamekuwa wakienda mahakamani kuweka zuio na kwamba kwa kuwa kumetokea janga kama la mafuriko, serikali imeanza kuchukua hatua haraka.

“Sheria ya ardhi inasema mtu akikaa zaidi ya miaka 10 akajenga makazi yake huwezi kumuondoa eneo lake mpaka umlipe fidia,” alisema Lyimo.

Wakati huo huo, kiasi cha Sh. 3,544,682,014 zilichangwa na serikali, watu binafsi, taasisi, makampuni na mashirika mbalimbali kwa ajili ya kusaidia watu waliopatwa na maafa ya mafuriko mkoani Dar es Salaam Desemba mwaka jana na kuhamishiwa Mabwepande.

Lyimo alisema kati ya fedha hizo, Sh. milioni 964 zilitolewa na Wizara ya Maji na kutumika kuweka huduma ya maji wakati Wizara ya Nishati na Madini ilichangia Sh. milioni 672 kuweka umeme.

Alisema katika mafuriko hayo, watu 41 walipoteza maisha na kwamba kaya 553 zilihamishiwa Mabwepande kwa awamu ya kwanza na kaya 457 zilihamishwa katika awamu ya pili na kugawiwa viwanja kwa ajili ya kujenga makazi yao.
Naye Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ali Kessy Mohamed, alisema kuna haja ya kuwa na kitengo maalum kwa ajili ya kuwashitaki watu wanaojenga kwa makusudi katika maeneo ya mabondeni na kusubiri mafuriko yatokee ili walipwe fidia.

“Watu wanajenga mabondeni kwa makusudi ili walipwe fidia, kwanini wasikamatwe na kushitakiwa, tunakuwa nchi ya siasa siasa tu?” aliuliza Kessy.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Abdul Marombwa, alizitaka halmashauri zote za Jiji la Dar es Salaam kujipanga na kuainisha maeneo ambayo hayapaswi kujengwa.

Serikali kwa muda mrefu imeshindwa kuwaondoa wakazi wanaoishi mabondeni katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Hata hivyo, baada ya maafa yaliyosababishwa na mafuriko ya Desemba mwaka jana, viongozi wake wamekuwa wakitoa kauli mara kwa mara kwamba nyumba zote zilizojengwa mabondeni zitabomolewa baada ya zoezi la kuwahamishia waathirika wote Mabwepande.