Tume ya uchaguzi ya Misri inasema kuwa itatangaza Jumapili matokeo ya uchaguzi wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais uliofanywa mwisho wa juma lilopita.
Tume imekuwa ikisikiliza malalamiko ya wagombea wawili - Mohamed Mursi wa chama cha Muslim Brotherhood, na waziri mkuu wa zamani, Ahmed Shafiq.

Kila mmoja kati ya wagombea hao wawili amedai kuwa ameshinda, na kwamba ataunda serikali ya kuleta umoja nchini.

Wafuasi wa Muslim Brotherhood wamekuwa wakiandamana katika medani ya Tahrir kati ya mji wa Cairo, kudai matokeo yatangazwe.

Mwandishi wa BBC mjini Cairo anasema kila upande unaogopa kutatokea maafa endapo upande wa pili atashinda.