BAADA ya kutamba kwa muda mrefu katika muziki wa kizazi kipya nchini, msanii
nyota wa muziki huo, Naseeb Abdul ‘Diamond’ amesema anafikiria kujitosa katika
muziki wa taarab.
Diamond alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, amefikia
uamuzi huo kutokana na kuvutiwa na muziki huo wa taarab.
Mshindi huyo wa tuzo
mbalimbali za muziki za Kilimanjaro amesema, anajua uamuzi wake huo
utawashangaza mashabiki wengi, lakini ni jambo la kawaida kwa msanii.
Diamond
alisema hadi sasa anaamini hana mpinzani katika muziki wa kizazi kipya na hakuna
msanii anayeweza kufikia kiwango chake hapa nchini.
“Najua watu watanishangaa
na kuniona mtu wa ajabu, lakini nimefanya hivyo kwa sababu sina mpinzani katika
muziki wa kizazi kipya,”alisema.
Diamond alisema ameamua kupiga miondoko
tofauti ya muziki kutokana na kipaji alichonacho katika fani hiyo, ambayo
imempatia umaarufu mkubwa.
Kutokana na kipaji chake hicho, Diamond alisema
hakuna kitu anachoshindwa kukifanya katima muziki.
“Bado sijaanza rasmi
kupiga muziki wa taarab, ninachokifanya kwa sasa ni kufanya tathmini ya soko
lake ili kuona kama unaweza kuniletea mafanikio kama ilivyo kwa muziki wa bongo
fleva,”alisema msanii huyo.
“Naweza kufanya kila aina ya muziki kwa sababu
nina kipaji cha kuimba nyimbo aina zote, hivyo endapo nitafikia muafaka, naweza
kufanya kitu hicho ingawa mashabiki wangu watashtuka sana,” alisema.
Diamond
alikiri kuwa, muziki wa kizazi kipya umemfanya ajulikane sehemu nyingi duniani,
ikiwa ni pamoja na kupata manufaa mbalimbali kimaisha kwa kuishi kwenye nyumba
nzuri na kumiliki magari ya kifahari.
Msanii huyo mwenye haiba ya kuvutia
alisema, kwake muziki ni kazi kama zilivyo kazi zingine hivyo amekuwa akifanya
kazi zake kwa malengo.
Alisema siri kubwa ya muziki wake kuwateka mashabiki
wengi ndani na nje ya nchi ni kufanyakazi zake kwa kujituma na pia kujiwekea
malengo.
"Sifanyi muziki kwa ajili ya kujifurahisha, kutafuta pesa na
kuwaacha mashabiki wangu wabaki na kiu ya burudani,”alisema
Diamond.
“Ninapofanya muziki nahakikisha kuwa, nakata kiu ya mashabiki wangu
kwa kuwapa burudani wanayoihitaji,”aliongeza.
Katika kufanikisha hilo,
Diamond alisema amekuwa na utaratibu wa kushirikiana na watu mbali mbali kwa
vile anaamini sio rahisi kuweza kufanya kila kitu peke yake.
Alisema miongoni
mwa watu, ambao wamekuwa wakimpa ushirikiano mkubwa katika kazi zake ni wacheza
shoo kwa vile wamekuwa wakibuni vionjo vipya kila kukicha.
"Siwezi kuwa na
ubahili ninapofanya kazi na hili ndilo lililonifanya nizidi kusonga mbele katika
kazi ya muziki. Ili upate ni lazima utoe na ili uwafurahishe mashabiki wako ni
lazima uzingatie kanuni hizo,”alisema.
0 Comments