Meya wa Manispaa ya Kinondoni,Mh. Yusuph Mwenda ambaye pia alikuwa Mgeni rasmi akizungumza katika tamasha la uhamasishaji wa Wananchi kwa ajili ya kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya, lililozinduliwa mwishoni mwa wiki katika Viwanja vya Mburahati kwa Jongo, Dar es Salaam.
Kiongozi wa Chama Cha Wanafunzi waliokuwa wanafadhiliwa na Shirika la Ford Foundation la Marekani, Harold Sungusia akifafanua mbele ya Wanahbari kuwa wameamua kuzindua tamasha hilo kwa jiji la Dar Es Salaam kwa madhumuni ya kuwahamasisha jamii iweze kujua haki zao kwa kupitia burudani mbalimbali.

=========== ======= =====
TAMASHA la uhamasishaji wa Wananchi kwa ajili ya kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya, limezinduliwa mwishoni mwa wiki katika Viwanja vya Mburahati kwa Jongo, Dar es Salaam. Tamasha hilo ni maalum kwa ajili ya Wananchi kupata fursa ya kutambua haki zao kwa kupitia burudani.

Akizungumza jijini Dar mwishoni mwa wiki kwenye uzinduzi wa tamasha hilo, Kiongozi wa Chama Cha Wanafunzi waliofadhiliwa na Shirika la Ford Foundation la Marekani, Harold Sungusia alisema kuwa wameamua kuzindua tamasha hilo kwa jiji la Dar Es Salaam kwa madhumuni ya kuwahamasisha jamii iweze kujua haki zao kwa kupitia burudani mbalimbali.

Alisema kuwa baada ya uzinduzi wa tamasha hilo, pia wanaandaa tamasha lingine ambalo litafanyika katika Viwanja vya Biafra Dar es Salaam na baadaye kulipeleka mikoa yote ya Tanzania bara. Alisema kuwa sanaa wanazotumia kufikisha ujumbe kwa jamii ni pamoja na ngoma, maigizo, tamthilia na sarakasi. Alisema kuwa watakuwa wanatumia mfumo wa burudani mbalimbali kwa ajili ya kuwakusanya watu zaidi na kuwapatia elimu kwa kupitia burudani hizo.

Alisema kuwa lengo lao ni kutoa elimu ya kwa jamii kwa ajili ya kutoa maoni juu ya Katiba mpya ambapo wao wameamua kuanzia ngazi za chini kutokana na watu wengi kutokuwa na uelewa mzuri juu ya Katiba Mpya.

"Tumeamua kuzindua tamasha hili ambalo litakuwa linaendeshwa na burudani kwa asilimia kubwa ambapo lengo letu ni kutoa elimu kwa jamii juu ya kutoa maoni kuhuhu Katiba Mpya" alisema. Katika tamasha hilo Mgeni Rasmi alikuwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda alisema kuwa watu wengi hawajui maana ya Katiba hivyo wanashindwa kutambua haki zao.

Alisema kuwa kupitia tamasha hili ambalo litafanyika pia kila mkoa, litatoa fursa ya watu kujua haki zao za msingi kupitia katika burudani mbalimbali zitakazokuwa zinatolewa kupitia matamasha hayo.