Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) umewatuhumu baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaotoka Chama Cha CCM na kutishia kuwanyanganya kadi za uanachama kutokana na kuwa sawa na ‘Mamluki’ katika matendo yao. Kauli hiyo imetolewa juzi katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama hicho uliofanyika viwanja vya Komba wapya Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ambapo Katibu wa UVCCM Wilaya ya Mjini, Mohammed Ali Khalfan alisema CCM inaweza kuwanyanganya kadi za chama hicho viongozi hao.Alisema viongozi hao ambao ni wajumbe wa baraza la wawakilishi zanzibar wameonekana kuwa na mtazamo tofauti na chama chao na hivyo kutaka wachukuliwa hatua ikiwemo kunyanganywa kadi za chama hicho cha CCM.
Katibu huyo alisema wapo Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaokwenda kinyume na maadili ya chama hicho ambao amewafananisha kutokuwa na tofauti na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam Zanzibar (JUMIKI).
“Ndugu Mwenyekiti tunaomba utupelekee salamu zetu kwa hawa Wawakilishi wetu wa CCM ambao ni mamluki waambie Umoja wa Vijana wa (CCM) tunawajuwa wanavyofanya na ipo siku tutawataja majina yao hadharani” Alitishia Katibu huyo wa Wilaya.

Katibu huyo alisema kwamba UVCCM inashangazwa na Wawakilishi hao wa CCM kupoteza mwelekeo kwa baadhi yao kuvuka mipaka ya imani ya Chama chao na kuunga mkono sera na itikadi isiyotokana na Chama hicho kikongwe hapa nchini.
“Mheshimiwa mgeni rasmi kama tulivyosema tufikishie salaam zetu kwa hao Wawakilishi wanaotokana na CCM, waambia itafika wakati tutawanyanganya kadi zetu kwa sababu hawatuwakilishii chama chetu” Alisisitiza Katibu huyo.
Huku akishangiriwa na waliohudhuria katika mkutano huo Khalfan aliwapongeza Wabunge wa CCM akiwataja kama viongozi wanaotetea imani, sera na itikadi ya chama chao ndani na nje ya Bunge, akitoa wito kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CCM kuiga mfano huo juu ya utetezi wa kulinda na kuhifadhi Muungano.
Katibu huyo alisema faida za Muungano ni nyingi na itachukua muda kuzimaliza kuzitaja, lakini jambo la msingi kwa Wabunge na Wawakilishi kutetea kudumu kwa Muungano ambao sasa umetimiza miaka 48 tangu kuasisiwa kwake mwaka 1964.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mjini Borafia Silima Juma ambaye alikuwa ndiye mgeni rasmi katika mkutano huo, aliwakumbusha hasa vijana ulazima wa kuulinda Muungano huku akiwataka kuwapuuza watu wanaoubeza Muungano huo akisema haujawahusu.
“Hawa watu wanaotaka Muungano uvunjike waulizeni wameunda wao, Muungano bwana ni wetu sisi tangu zamani Afro Shiraz Party tulikuwa na imani yetu na ahadi za mwanachama ambazo ni pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ” Alisema Mwenyekiti huyo.
Akitoa historia Borafya aliwaambia wanachama wa chama hicho ambao wengi wao walikuwa ni vijana kwamba Chama cha ASP ndicho kilichoungana na TANU kuunda Chama cha Mapinduzi Februari 5 mwaka 1977 katika sherehe zilizofanyika uwanja wa Amaan Mjini Zanzibar ambapo Mwenyekiti wa kwanza wa Chama hicho alikuwa Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere na Makamu Mwenyekiti wake, Aboud Jumbe Mwinyi.
Borafia alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni matokeo ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 Mapinduzi ambayo ndio yaliyokata mizizi ya Utawala mkongwe wa Kisultan Zanzibar hivyo CCM itaulinda kwa gharama yoyote Muungano huo uliopo na hakuna sababu ya kuogopa watu wenye kupinga.
Mbali na kuwaeleza wanachama hao suala la muungano, Borafya ambaye anatambulika kwa kupiga watu vijembe na kutumia lugha ya matusi wakati mwengine anapokasirika aliwashambulia viongozi wa jumuiya ya UAMSHO kutokana na elimu wanayoitia kwa umma na kusema kwamba jumuiya hiyo haina nguvu za kuwashawishi wananchi kuvunja Muungano na khasa kwa kuwa dhamira ya jumuiya hiyo inatambulika.
Bila ya kutaja dhamira ya jumuiyo hiyo, Borafya aliwataka wana CCM kupuuza maneno yatakayotolewa na viongozi wengine wasiokuwa CCM na kuwataka vijana kuwa macho na kuutetea Muungano akisema una faida kubwa ingawa hakutaja faida lakini alisema faida zipo nyingi na Zanzibar inanufaika na faida hizo.
Kwa upande wake Kada maarufu wa CCM Zanzibar, Baraka Mohammed Shamte alielezea faida mbalimbali za Muungano kiuchumi, kisiasa, na kijamii, lakini pia hasara ikiwa utavunjika na kuonya kwamba wanaoleta chokochoko hawaitakii mema Zanzibar wala Tanganyika .
Shamte alisema uhuru wa Zanzibar wa mwaka 1963 haukuwa uhuru wa kweli kwani badala ya kukabidhiwa vyama vya ZNP na ZPPP Serikali ya Uingereza ilimkabidhi Sultan wa Zanzibar kwa kuwa ndiye waliyekuwa wakimlinda, hivyo kufanya ASP kufanya mapinduzi Januari 1964.
“Mimi baba yangu ndie aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza katika uhuru bandia wa mwaka 1963 nafahamu mambo mengi kuliko nyie kwanza wengi wenu ni watoto wadogo hasa nyie Uamsho hamjui lolote, kwa hivyo Muungano utadumu mtake mistake” Alisisitiza Shamte huku akishangiriwa na wanachama hao.
Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) imeingia katika malumbano tokea kuanza kwa suala la katiba ambapo kila upande umekuwa ukifanya mikutano ya hadhara na kila upande kuwa na kauli yake wakati Uamsho wakitaka kuvunjika kwa muungano ambapo CCM wanasema muungano huo hauvujiki.
Uamsho imekuwa ikifanya mihadhara ya nje lakini serikali ilipiga marufuku mihadahara hiyo na jeshi la polisi kuwatawanja waumini hao kila mwisho wa wiki ambapo sasa wanatakiwa kufanya mihadhara yao ndani ya misikiti wakati chama cha CCM kikiwa kimesitisha mikutano yake na ndio kwanza kimeanza kufanya sasa mikutano hiyo tokea kupigwa marufuku na jeshi la polisi.