Utafiti mpya uliofanywa sehemu mbali mbali za dunia, kutaka kujua wapi watu
wanaficha fedha zao kukimbia kodi, umegundua kuwa dola kama trilioni 20,
zimefichwa nchi za ng'ambo, mbali ya macho ya maafisa wanaotoza kodi.
Ripoti hiyo imeandikwa na shirika la utetezi, Tax Justice Network, ambayo
inasema kuwa tofauti baina ya matajiri na maskini ni kubwa kuliko
ilivofikiriwa.
Dola trilioni 21 ni sawa na pato la mwaka la Marekani nzima pamoja na
Japani.
Tax Justice Network inafikiri fedha zilizofichwa ng'ambo zinaweza kuwa zaidi
ya hizo.
Ripoti yao inaonesha jinsi matajiri wakubwa wanavohamisha fedha na kuziweka
kwenye nchi zinazoweka siri, kama Uswiswi na Visiwa vya Cayman, kwa kupitia
mabenki ya kibinafsi.
Ripoti piya inaeleza kuwa nchi zenye utajiri wa mafuta, kama Urusi na
Nigeria, ndio hasa kwenye mtindo wa fedha kutoweka na kuvushwa, badala ya
kuwekezwa nchini.
Utafiti huo unamaliza kwa kusema wanasiasa sehemu mbalimbali za dunia,
wanategemea kuwa fedha hata zikiwa kwa watu wa juu, zitavuja hatimae na
kuwafikia maskini - ripoti inasema hayo hayatokei tena.

0 Comments