Gladness Mallya na Hamida Hassan
SOO juu ya soo! Baada ya mkali wa Bongo Fleva, Nasibu ‘Diamond’ Abdu kumchana baba yake, Abdu Juma katika gazeti dada na hili Ijumaa, mzazi huyo ameibuka na kumtaka mwanaye asitumie jina lake tena, Risasi Mchanganyiko linashuka kwa kujiamini.
Akizungumza kwa uchungu hivi karibuni, nyumbani kwake Magomeni, Dar, mzee Abdu alisema kitendo cha Diamond kumkana kwenye vyombo vya habari na kusema kuwa yeye siyo baba yake kilimuudhi sana na haoni sababu ya kuendelea kutumia jina lake.
SAUTI YA MZEE ABDU KUTOKA MAGOMENI
“Nasibu (Diamond) ni mwanangu na hilo jina nimempa mimi, nimemlea mwenyewe na kumpeleka shule, lakini leo ananikana. Kama ndivyo, aache kutumia jina langu.
“Nilimtumia meseji baada ya kuona gazeti hilo mtaani nikamwambia atafute jina lingine maana ameshasema hanitambui kama baba yake. Namshangaa sana huyu mtoto, hata sitaki kumsikia lakini ipo siku nitamtafuta nimweleze kwa mdomo.
“Sina shida na umaarufu wake kama anavyodhani, yeye aendelee na mambo yake, kwanza hana faida na mimi, si amedai aliyemlea ni mama yake? Basi aendelee naye sitaki kupigizana naye kelele,” alisema mzee Abdu.
KUMBE DIAMOND ALIWAHI KUMPELEKA WEMA KWA MZEE ABDU!
Katika kuthibitisha kwamba, Diamond anatambua yeye ni baba yake, mzee Abdu alisema, alipomvalisha Wema Sepetu pete ya uchumba alimpeleka nyumbani kwake kumtambulisha.
“Diamond alikuja kunitambulisha Wema kuwa ndiye mchumba wake ikiwa ni baada ya kumvisha pete na tulipiga naye picha,” alisema.
Hata hivyo, alikataa kutoa picha hizo kwa waandishi wetu ili zitumike gazetini.
Aliongeza: “Mama yake huwa tunaongea vizuri tu, hata siku hiyo (aliyomwandikia meseji Diamond) nilimpigia mzazi mwenzangu na kumweleza, akaniambia niachane na mambo ya magazeti na redio, mimi nitabaki kuwa baba yake.
“Jambo hilo sikubaliani nalo hata kidogo, kwa sababu tayari amenidhalilisha, hata mtaani kwangu watu wanajua kuwa mimi ni baba yake na bado wanaendelea kuniita Baba Diamond... naitika kwa shingo upande tu,” alisema Abdu.
AMWACHIA MUNGU
“Diamond amefanya kitu kibaya na anatakiwa kujua kuwa nimeumizwa sana na kitendo chake, lakini sina namna. Mimi namwachia Mungu, yeye ndiye anayejua kuwa ni mwanangu au lah.
“Mzazi yeyote lazima ataumizwa na maneno mabaya ya mwanaye kama alivyofanya yeye. Si maungwana watu wengine kuiga tabia ya namna hii. Diamond amenidhalilisha,” alisema.
0 Comments