Na Gladness Mallya
KUTOKANA na kuzidi kwa wimbi la mastaa wa Kibongo kuugua na kulazwa mwaka 2012 katika hospitali mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi, daktari aliyeomba hifadhi ya jina lake ameeleza sababu na kusema wapo hatarini kuzeeka mapema, Amani lina ripoti kamili.
Gazeti hili lilizungumza na daktari huyo anayefanya kazi katika hospitali moja kubwa hapa nchini ambapo alisema sababu zinazowafanya mastaa wengi kukumbwa na magonjwa mbalimbali ni uzee, vyakula wanavyokula, kutofanya mazoezi na kutokuwa na mazoea ya kupima afya zao mara kwa mara.
“Unajua mastaa hawa wakishapata umaarufu, basi wanabweteka. Hawafanyi mazoezi, wanapenda vyakula vyenye mafuta mengi wakidhani wanakula
vizuri kumbe wanajiharibu,” alisema dokta huyo.
Mastaa wengi waliolazwa kwa mwaka 2012 walikuwa wakisumbuliwa zaidi na magonjwa kama presha, tumbo, kifua, malaria na mengine mengi ambapo hapa tunakuletea listi ya mastaa hao na magonjwa yaliyokuwa yanawasumbua.
WEMA SEPETU
Hivi karibuni Wema alilazwa katika Hospitali ya Heamed iliyopo Upanga, Dar akisumbuliwa na tatizo la kubanwa kifua ambapo hali yake ilikuwa mbaya kiasi cha kuwafanya Watanzania wamuombee.
NASIBU ABDUL ‘DIAMOND’
Diamond aliugua ghafla akiwa nyumbani kwake Sinza-Mori, Dar ambapo alikimbizwa kwenye Hospitali ya Heamed na kulazwa akisumbuliwa na homa kali na uchovu uliosababishwa na kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika.
SAID NGAMBA ‘MZEE SMALL’
Mkongwe huyo wa maigizo na filamu anasumbuliwa na ugonjwa wa kupooza ambapo alilazwa Muhimbili, Dar na baadaye aliruhusiwa lakini hadi sasa bado ni mgonjwa.
COLETHA RAYMOND ‘KOLETA’
Hivi karibuni mwigizaji huyo alilazwa kwenye Hospitali ya Kairuki iliyopo Mikocheni, Dar akisumbuliwa na ugonjwa wa kidole tumbo ‘appendix’ ambapo alifanyiwa upasuaji na kupoteza fahamu kwa takribani saa saba.
TAMRINA POSHI ‘AMANDA’
Wiki mbili zilizopita Amanda alilazwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dodoma kutokana na kusumbuliwa na presha kushuka.
RUTH SUKA ‘MAINDA’
Mwigizaji Mainda alilazwa kutokana na kusumbuliwa na presha ya kushuka ambapo alidondoka ‘lokesheni’, tatizo hilo likaendelea kumsumbua mara kwa mara.
JUMA KILOWOKO ‘SAJUKI’
Mwigizaji Sajuki alilazwa nchini India akisumbuliwa na uvimbe tumboni ambapo baada ya matibabu alirejea Bongo na mpaka sasa bado hajawa fiti vya kutosha.
WASTARA JUMA
Mwigizaji Wastara ambaye ni mke wa ndoa wa Sajuki naye alilazwa nchini India wakati alipokwenda na mumewe kwa ajili ya kumhudumia.
HUSNA IDD ‘SAJENTI’
Wiki iliyopita mwigizaji huyo alilazwa huko kwao, Kondoa-Irangi, Dodoma akisumbuliwa na homa ya mapafu.
0 Comments