Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akiufungua mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Kitope uliofanyika Kinduni Wilaya ya Kaskazini B.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Kitope wakiwa tayari kwa ajili ya uchaguzi wa kuwachagua Viongozi wao watakaowaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Othman Khamis Ame – Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi amewaomba Wanachama wa Chama hicho ambao tayari wameshaamua kwenda tofauti na sera za chama hicho katika mfumo wa muundo wa Muungano ni vyema wakakiacha chama hicho kwa heshima na Taadhima.
Balozi Seif akiwa pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mbunge wa Jimbo la Kitope ametoa ombi hilo wakati akiufungua mkutano Mkuu wa uchaguzi wa CCM Jimbo la Kitope uliofanyika katika Ofisi ya Jimbo hilo iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini B.
Balozi seif alisema wakati umefika kwa wanachama wa CCM wasiozikubali sera za chama hicho ambazo zimepata ridhaa ya Wananchi waliowengi kuongoza Nchi hii itapendeza kama watarejesha kadi za chama hicho mara moja.
Aliwataka Wanachama wa chama cha Mapinduzi kujizatiti katika kuhakikisha Nchi inaendelea kubakia kuwa ya amani na salama muda wote.
“ Wale wanaotaka kutuvurugia chama chetu na Muungano wetu waturejeshee kadi zetu. Kwa nini wanachama haio wanasubiri mpaka wajadiliwe kwenye Vikao vya chama au vile vikao vya maadili? Ya nini kutuvurugia chama chetu wakati nafasi za kung’atuka ipo wazi? Aliuliza Balozi Seif.
Alisema Taifa hivi sasa linapita katika kipindi kigumu kutokana na baadhi ya vikundi kujaribu kushawishi wananchi na hasa Vijana kujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani.
Aidha alieleza kwamba Wanachama hao hawana budi kufikiria kupanga safu makini itakayoendeleza na kusimamia vyema uendeshaji wa chama pamoja na taifa kwa ujumla.
Balozi Seif alitahadharisha kwamba hivi sasa jamii inashuhudia matusi ya nguoni yanayoendelezwa na baadhi ya makundi ya watu dhidi ya Viongozi wa Serikali na Chama hali ambayo kama Jamii hiyo haitakuwa makini Taifa linaweza kutumbukia katika fujo na hatimae maangamizi.
“ Tunakotoka kubaya sote ni mashahidi, kwa sababu familia na hata ndugu wa karibu walikuwa hawaulizani hali na hata maziko hawaendeani. Kwa kweli tusifikie tabia hii kuiruhusu irejee tena”. Alifafanua Balozi Seif.
Alisisitiza kwamba Chama cha Mapinduzi kitaendelea kuunga mkono mfumo wa uongozi wa Serikali mbili nchini Tnaznia na kuamini kwamba Mwanachama ye yote wa chama hicho anayejiamini ataunga mkono mfumo huo.
Akizungumzia ujenzi na uimarishaji wa majengo ya Matawi ya chama Balozi Seif alieleza kuwa mkazo utaendelea kuwekwa ili kukamilisha matawi matatu yaliyobakia ndani ya Jimbo hilo kati ya matawi yote 20.
Alisema hatua hiyo imelenga kwenda sambamba na mfumo wa chama cha Mapinduzi ya kuwa na Ofisi zenye hadhi inayokubalika.
Akitoa Taarifa ya utekelezaji wa chama katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Katibu wa CCM Jimbo la Kitope Nd. Khamis Khamis alisema uongozi wa chama hicho umejipangia kuongeza idadi ya wanachama watatu kwa kila shina.
Nd. Khamis alisema hatua hiyo inalenga zaidi kuimarisha nguvu na uhai wa chama katika utekelezaji wa sera na ilani zake.
Katika mkutano huo wajumbe hao wamemchagua Ndugu Zamir Makame kuwa Mwenyekiti Mpya wa Jimbo la Kitope, Katibu ni Nd. Khami Khamis, Katibu Mwenezi ni Nd.Hamisa Yussuf na Uchumi na Fedha ni Nd.Juma Fadhil. Wajumbe wa Kamati ya Siasa ni Ndugu Hilika Fadhil, Nd. Asha Suleiman,Maryam Haji naMwinyi Mahfoudh. Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa ni Nd. Ali Ameir, Ali Khamis na Nd.Juma Makame.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya ni Nd. Abdulla Seif, Nd, Maryam Haji, Nd.Christina Benjamin, Nd. Ali Haji na Nd. AbdullaVuai.
Wajumbe wa Halmashauri ya Jimbo ni Nd. Asha Suleiman, Nd. Hilika Fadhil, Nd. Hamisa Taufiq, Nd. Mwinyi Mahfoudh na Nd. Maryam Haji.