LEO Simba itacheza mechi ya kirafiki na klabu ya soka ya Oljoro JKT katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta jijini Arusha.
Mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya Ligi Kuu ya Tanzania inayotarajiwa kuanza baadaye mwezi ujao.
Hii itakuwa mechi ya pili ya kirafiki ya Simba kucheza jijini Arusha baada ya ile ya majuzi dhidi ya Mathare United ya Kenya.
Oljoro JKT imetoka kwenye michuano ya timu za majeshi hapa nchini ambapo ilichukua nafasi ya kwanza pamoja na Ruvu JKT.
Kocha Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amesema atatoa nafasi kwa wachezaji wengi kwa kadri itakavyowezekana kwenye pambano hilo.
Viingilio vitakuwa ni Sh 5,000 kwa VIP A, Sh 3,000 kwa VIP B na Sh 2000 kwa VIP C. Kiingilio kwa watoto kitakuwa ni Sh 1000.
Felix Mumba Sunzu.
Mchezaji huyu ameondoka nchini jana kuelekea jijini Lubumbashi, DRC kuhudhuria msiba wa dada yake ambaye alifariki dunia majuzi jioni nchini humo.
Dada huyo alikuwa amekwenda kumtembelea mdogo wa Sunzu, Stopila, ambaye anachezea klabu ya soka ya TP Mazembe siku sita zilizopita lakini akakumbwa na umauti kutokana na ugonjwa wa Malaria iliyopanda kichwani (Cerebral Malaria).
Uongozi wa Simba umetoa pole kwa familia ya Sunzu pamoja na kufanikisha kuondoka kwa haraka kwa mchezaji huyo ili akaungane na familia yake.
Sunzu atarejea nchini baada ya kumaliza maziko na klabu ya Simba inaomba vyombo vya habari na wadau wengine kumpa nafasi ya kuomboleza msiba huu mzito kwake binafsi, kwa familia yake na Simba.
Mola na aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi. Amen
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC