Wabunge wa Somalia
Waziri wa zamani nchini Somalia,Mohamed Osman Jawari amechaguliwa kama spika wa bunge katika mchakato wa amani wa umoja wa mataifa wa kumaliza vita vya muda mrefu nchini Somalia.

Bwana Jawari alichaguliwa na wabunge walioapishwa wiki jana . Washindani wenzake walijiondoa kutoka kwa kinyang'anyiro hicho.

Osman anatoka ukoo wa Rahanweyn na hatua hiii ina maana kuwa spika mtangulizi wake, Shariff Hassan Sheik Adan, huenda asichaguliwe kama rais wakati uchaguzi utakapofanyika katika siku chache zijazo.

Bwana Adan pia anatoka kwenye ukoo wa Rahanweyn ambako mamlaka hugawanywa bila wasiwasi.Kawaida rais huchaguliwa kutoka kwa ukoo tofauti na spika wa bunge


Adan alikuwa mpinzani mkubwa wa rais anayeondoka Sheikh Sharif Sheikh Ahmed.

Jawari vile vile alikuwa waziri katika utawala wa Siad Barre, ambaye serikali yake ilikuwa ya mwisho kuitawala Somalia kabla ya yeye kung'olewa mamlakani mnamo mwaka 1991.

Bwana Ahmed, ambaye ni mwanasiasa mwenye msimamo wa kadri, ni mmoja wa wagombea mashuhuri katika king'anyanyiro cha rais.

Maafisa wa usalama wanaounga mkono serikali, wameweza kudhibiti maeneo yaliyokuwa zamani ngome za Al Shabaab. Hata hivyo, bado watu wenye siasa kali wanadhibiti maeneo ya kusini na kati mwa Somalia.