Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa Simba umekubali kuwa kweli upo tayari kumsajili kiungo nyota wa Azam FC, Mrisho Ngassa, lakini umesisitiza dau la dola 50,000 (zaidi ya Sh milioni 75) ni kubwa sana.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, ameliambia Championi Jumatano kuwa, Kocha Mkuu, Milovan Cirkovic, amekuwa akisisitiza kuhusu kumnasa Ngassa.
“Tatizo ni dau la Azam, tuliwahi kupata maelekezo ya kocha. Mara moja tukaenda Azam na kuwapa ofa yetu lakini wakakataa.
“Kweli tunamhitaji na kocha wetu amesisitiza anamhitaji lakini kiasi walichotangaza hakika kipo juu sana. Hatutaweza, ila wakipunguza tunaweza kufanya biashara,” alisema Kaburu.
Azam FC iliyoingia fainali ya michuano ya Kombe la Kagame ikiwa inashiriki kwa mara ya kwanza, imetangaza kumuweka sokoni Ngassa ambaye ilimnunua kutoka Yanga kwa kitita cha jumla ya Sh milioni 98.
Hivi karibuni, gazeti la Championi lilitoa picha za Ngassa akivaa na kuibusu jezi ya Yanga pia alishangilia bao lake dhidi ya AS Vita ya DR Congo na mashabiki wa Yanga.
Kitendo hicho kiliukasirisha uongozi wa Azam FC ambao umesisitiza kuwa, Ngassa ameonyesha hana mapenzi na klabu hiyo na anaweza ‘kusepa’.