Hali ya wasiwasi Mombasa
Hali ya wasiwasi imetanda mjini Mombasa Kenya baada ya kuzuka vurugu kwa siku ya pili kufuatia ghasia siku ya Jumatatu zilizosababishwa na wafuasi wa Aboud Rogo aliyekuwa mhuburi wa kiisilamu huko Mombasa.

Ghasia zilitokea baada ya kuuawa kwa mhubiri huyo mashahuri ambaye pia alikuwa mshukiwa wa ugaidi.
Vijana walirushia mawe magari ya polisi na kuweka vizuizi katika mtaa wa Saba Saba, mjini Mombasa.

Katika mtaa wa Majengo, polisi walitumia risasi za mipira kuwatawanya vijana waliokuwa wanaandamana.Inaarifiwa kuwa mtu mmoja alidungwa kisu katika vurugu hilo.
Hapo jana wafuasi wa Rogo walizua vurugu na kusababisha uharibifu mkubwa baada ya kiongozi woa kuuawa na watu wasiojulikana akiwa safarini kumpeleka mkewe hospitalini.


Mwandishi wa BBC mjini Moambasa alielezea kuona makundi ya vijana wakipambana na polisi waliokuwa wanatumia gesi ya kutoa machozi kujaribu kuwatawanya. Mtu mmoja alifariki hapo jana na wengine wengi kujeruhiwa katika ghasia za hapo jana usiku huku makanisa yakivamiwa.

Maduka na sehemu zingine za biashara zimeharibiwa vibaya na kuporwa hadi maafisa wa polisi walipofika katika eneo hilo kuweza kudhibiti hali ya usalama.

Aboud Rogo alikuwa ametuhumiwa kwa kusajili wapiganaji wapya kwa niaba ya kundi la wanamgambo la Alashabaab pamoja na kufadhili kundi hilo.

Aboud Rogo Mohammed alikuwa kwenye orodha ya Marekani na ile ya Umoja wa mataifa ya watu wanaosaidia katika harakati za kundi la wanamgambo wa kiisilamu nchini Somalia la al-Shabab

Kulingana na ripoti ya umoja wa mataifa, Rogo alisaidia kundi la al-Shabab kusajili makurutu wapya. Pia alikuwa anakabiliwa na madai ya njama ya mashambulizi dhidi ya kanisa moja mjini Mombasa.

Kwa mujibu wa taarifa, bwana Rogo alipigwa risasi wakati akiendesha gari lake katika mtaa a Bamburi mjini humo.

Aboud Rogo Mohammed aliwekwa nwenye orodha ya Marekani ya watu waliowekewa vikwazo mwezi Julai,kwa kujihusisha vitendo vyinavyohujumu amani na usalama nchini Somalia.

Baraza la usalama la umoja wa mataifa lilimwekea vikwazo vya usafiri na pia kupiga tanji mali zake mwezi Julai, wakisema kuwa alitoa ufadhili wa kifedha, usafiri na kusaidia kundi hilo kwa vifaa vya kisasa.

Ilimtuhumu kwa kuwa kiongozi maalum wa vuguvugu la al- Hijra nchini Kenya ambao pia wanajulikana kama Muslim Youth Center, ambalo linatazamiwa na wengi kama lililo na uhusiano wa karibu na al-Shabab.

Umoja wa mataifa ulisema kuwa bwana Rogo alitumia kundi hilo kama njia moja ya kuwatia watu kasumba ya siasa kali hasa wanaoongea lugha ya kiswahili kwa lengo la kufanya mashambulizi ya kigaidi.