Julius Melama akiwahutubia wafanyakazi wa migodi waliokuwa
wanagoma
Mwanasiasa mwenye utata wa Afrika Kusini Julius Malema
amefikishwa mahakamani akikabiliwa na shtaka la kujipatia pesa kwa njia haramu,
huku mamia ya wafuasi wake wakikusanyika nje ya mahakama kumuunga mkono.
Ingawa mahakama ilimwachilia kwa dhamana.
Seng'enge zilizungushwa katika eneo la mahakama hiyo iliyopo Polokwane, mji
mkubwa wa jimbo analotokea mwanasiasa huyo,Limpopo.
Malema pia anatuhumiwa kwa kutumia vibaya wadhifa aliokuwa nao kama mkuu wa
chama tawala cha African National Congress (ANC) tawi la vijana.
Wafuasi wake wanasema mashtaka hayo yameshinikizwa kisiasa.
Wakiimba na kucheza nje ya mahakama hiyo wafuasi wengi wa chama hicho cha ANC
tawi la vijana walishikilia mabango yaliosema 'Muacheni kiongozi wetu'.
Kuna maafisa wengi wa usalama lakini hali ni tulivu.
Julius Malema na washirika wake wa kibiashara wanashutumiwa kwa kufaidi
kutokanana na mikataba ya serikali katika jimbo la Limpopo, tuhuma ambazo
anazikana. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 31 pia anachunguzwa katika kesi
tofauti ya ukwepaji kulipa ushuru.
Malema ni maarufu sana Afrika kusini kwa ukakamavu wake wa kutetea maslahi ya
wananchi na maisha yake ya kifahari, huku akijitambulisha kama mpiganiaji uhuru
wa uchumi.
Alitimuliwa kwenye chama hicho tawala mnamo mwezi Aprili akishutumiwa kwa
kuzusha migawanyiko katika chama hicho.
Ni mkosoaji mkali wa a Jacob Zuma, hivi karibuni akimshutumu rais huyo kwa
alivyoushughulikia mgomo wa wachimba migodi wa Marikana.
Kwa mujibu wa mwandishi wa masuala ya Afrika, Andrew Harding, baadhi ya watu
Afrika kusini wanaamini anafikishwa haraka mahakamani, ikiwa ni chini ya wiki
moja baada ya kutolewa waranti ya kukamatwa kwake, ili kuimarisha nafasi ya
kisiasa ya Zuma.
Mwandishi wetu anaeleza kwamba huenda ikawa ni kesi ya muda mrefu, ambayo
huenda ikatoa nafasi ya kujulikana ukweli kuhusu suala hilo la rushwa, ambalo
watu wengi wanaamini inaitia nchi hiyo doa. |
0 Comments