Mama akiwa na mtoto wake anayekumbwa na njaa
Bara la Afrika limekuwa na mafanikio makubwa katika kupambana na njaa kuliko nchi zingine katika bara la Asia katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa ripoti kuhusu uzalishaji wa chakula duniani.
Uhaba wa chakula pamoja na utapia mlo vimepungua katika nchi nyingi barani Afrika, kulingana na ripoti hiyo inayotathmini viwango vya njaa duniani.

Lakini hali inasemekana kusalia kuwa mbaya zaidi katika nchi kama Eritrea na Burundi.

Ripoti hiyo inasema kwamba India ambayo imepiga hatua kiuchumi, imeshindwa kupambana vilivyo na tatizo la uhaba wa chakula.


Ripoti hiyo ambayo imegusia mambo mengi, pia inasema kuwa mashamba ya kuzalisha chakula yanaendelea kupunguka kwa sababu ya ongezeko la idadi ya watu.

Ripoti hiyo ambayo inatoa alama kwa nchi kulingana na idadi ya watu wanaokumbwa na utapia mlo, idadi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ambao wana utapia mlo na idadi ya vifo vya watoto hao, imeeleza hali ya njaa kuwa mbaya zaidi katika nchi ishirini.

Nchi hizo ni pamoja na Ethiopia, Chad, East Timor, Jamuhuri ya Afrika ya kati, Comoros, Sierra Leone, Yemen, Angola, Bangladesh, Zambia, Msumbiji, India, Madagascar, Niger, Dijibouti, Sudan na Nepal
Ingawa Haiti imekuwa ikipiga hatua, athari za tetemeko baya la ardhi ambalo lilitokea nchini humo mnamo mwaka 2010 , iliisababisha nchi hiyo kujijikota katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa njaa.

Kwa ujumla, kulingana na ripoti hiyo, hali hii ya Afrika kufanikiwa kuweza kukabiliana na tatizo la njaa, imetojitokeza hasa kwa sababu ya kupunguka kwa vita na kwamba serikali barani humo zimeanza kuwajibika katika kuimarisha afya ya watoto.