Askari wawili wa kulinda mbuga,pamoja na mwanajeshi mmoja wameuawa na waasi katika mbuga ya wanyama ya Virunga, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo .
Maafisa wanasema kuwa waasi watano pia waliuawa katika shambulizi ndani ya mbuga hiyo ambayo ndiyo iliyosalia pekee duniani kama hifadhi kwa sokwe.
Baadhi ya makundi ya waasi Mashariki mwa DRC ambayo yamejihami yana kambi zao katika msitu huo ambapo mara kwa mara huwinda wanyama kiharamu.

Zaidi ya walinzi 130 wa mbuga hiyo wameuawa ndani ya mbuga hiyo tangu mwaka 1996.

Kulingana na shirika la habari la Reuters waasi wa 23 ambao wana kambi zao humo, waliruhusu shughuli za kitalii kurejea katika hali ya kawaida.

Uasi wa mwaka huu ambao unaoendeshwa na M23, umesababisha watu 500,000 kupoteza makao yao.

Mkuu wa mbuga hiyo Emmanuel de Merode alisema kuwa walinzi waliokuwa wanasafiri chini ya ulinzi mkali, walivamiwa na waasi wa Mai Mai.

"walishambuliwa na kikundi cha waasi wa Mai Mai ambao walikuwa wengi kiasi. Mashambulizi dhidi yao yalikuwa makali kweli.'' aliambia shirika la habari la Reuters.

Mwezi Julai mwaka huu, makundi ya waasi yalikubali kuruhusu walinzi wa mbuga hiyo kuendelea na harakati za kuwatafuta sokwe waliosalia ndani ya mbuga hiyo.