Na Musa Mateja
MSANII wa filamu Bongo, Jacqueline Wolper Ijumaa iliyopita aliibuka kidedea kwenye lile shindano la kumsaka staa wa kike ambaye hajaolewa mwenye mvuto, The Ijumaa Sexiest Girl 2012 hivyo kuwafunika Wema Sepetu na Agnes Gerald ‘Masogange’ walioingia tatu bora.Fainali hiyo ilichukua nafasi ndani ya Ukumbi wa Dar Live uliopo Mbagala jijini Dar ambapo tukio hilo lilisindikizwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wa Bongo wakiwemo Ommy Dimpoz, Chid Benz, TOT Modern Taarab na wengineo.
Akimtangaza mshindi huyo, jaji mkuu ambaye naye ni msanii wa filamu, Mahsein Awadhi ‘Dokta Cheni’ alisema mwanzo wa shindano hilo walikuwepo washiriki zaidi ya 30 lakini mwishowe Wolper ameibuka mshindi.


Jacqueline Wolper akipozi na cheti chake baada ya kutwaa taji la Ijumaa Sexiest Girl 2012.
“Wolper ndiye mshindi na atazawadiwa kitita cha shilingi milioni 1 kutoka Global Publishers, atafanya ‘shopping’ ya shilingi milioni 1 kwenye duka la Shear Illusions lililopo Mlimani City jijini Dar na atapata ofa ya kupigwa ‘sopusopu’ kwenye saluni ya Perfect Lady iliyopo Kinondoni kwa mwaka mzima,” alisema Dokta Cheni.
Aidha, baada ya Wolper kutangazwa mshindi watu walilipuka kwa vifijo na nderemo kuonesha kukubali mwanadada huyo kuvaa taji hilo ambapo naye alipopewa nafasi ya kuzungumza, aliwashukuru kwa kumpigia kura hadi kuibuka mshindi.“Nawashukuru sana kwani nyie ndiyo wasomaji wa gazeti la Ijumaa na ndiyo mlionipigia kura, nawapenda wote kama mnavyonipenda,” alisema Wolper.
Shindano hilo liliendeshwa na Gazeti la Ijumaa ambalo ni dada wa hili na lilidhaminiwa na Ukumbi wa Dar Live, Shear Illusions pamoja na Perfect Lady Hair Saloon.