Meneja wa huduma za jamii wa Vodacom Foundation Mwamvua Mlangwa, akikabidhi mfano wa hundi ya fedha kiasi cha shilingi Milioni 20, kwa Mkurugenzi wa kituo cha Tanzania Mitindo House, Khadija Mwanamboka, Kwa ajili ya kuanzisha chuo cha mafunzo ya Mitindo kwa Watoto yatima.



Zaidi ya watoto yatima 50 waishio katika mazingira magumu watapata mafunzo ya ubunifu wa mavazi. Hii inafuatia kuanzikwa kwa kwa kituo cha ubunifu wa mavazi , (Mitindo House) kitakachokuwa chini ya Mwanamitindo maarufu, Hadija Mwanamboka.
Kituo hicho kitatoa mafunzo ya ushonaji, ubunifu wa mavazi, na utengenezaji wa vito mbalimbali kimefadhiliwa na mfuko wa huduma za jamii wa Vodacom (Vodacom Foundation)

Akizungumza baada ya kupokea mfano wa hundi ya shilingi Milioni Ishirini, Mkurugenzi wa kituo hicho, Hadija Mwanamboka, amesema kuwa lengo lao ni kuwawezesha watoto yatima waishio katika mazingira magumu na wasio na elimu kuweza kujitegemea kwa kujiajiri wenyewe kutokana na ujuzi watakao upata. 


“Tutatoa mafunzo kwa watoto wanaoishi katika vituo mbalimbali vya kulelea watoto yatima, yatakayo wawezesha kupata fursa ya kuonyesha vipaji vyao katika majukwaa ya sanaa na baadae kuwawezesha kujiajiri wao wenywe.”

“Mafunzo haya yatatolewa kwa mwaka mzima, wanafunzi ishirini na tano watapata mafunzo ya ushonaji na ubunifu wa mavazi na wengine 25 watapata mafuzno ya uchongaji wa vito mbalimbali na uchoraji,” alisema Hadija.

Kwa upande wake, Meneja wa Huduma za jamii wa Vodacom Foundation, Mwamvua Mlangwa amesema kuwa Vodacom Foundation imedhamiria kuboresha maisha ya jamii ya watanzania wanaoishi katika mazingira magumu.

 “Vodacom Foundation itaendelea kuwaunga mkono watanzania hususani wale wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwasaidia kujenga maisha yao na kusaidia kukua kwa uchumi wa nchi kupitia mipango mbalimbali tuliyonayo katika kitengo chetu,” alisema Mlangwa.