MKURUGENZI wa Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ International juzikati ameifungukia ishu ya aliyekuwa muimbaji wa bendi yake, Muumini Mwinjuma kuwa alikuwa na haki ya kuondoka kwani hakuwa na mkataba wowote na Kampuni ya Aset. Akizungumza na ‘kachala’ wa Funguka na Risasi ofisini kwake Kinondoni jijini Dar, Asha Baraka alisema tangu Muumini ajiunge na Bendi ya Twanga uongozi haukuwahi kuingia mkataba naye kwa sababu maalum ila alikuwa akipewa haki zake zote.“Muumini alikuwa anafanya kazi na Twanga kama vile kusaidiana tu kutafuta chakula cha kila siku, angalau alikuwa akipata mshahara na posho lakini hatukuwahi kuingia naye mkataba kwani bado uongozi ulikuwa unafuatilia baadhi ya mambo.” Funguka: Kwa hiyo unataka kuniambia Muumini alikuwa anapiga ‘deiwaka’ tu? Asha Baraka: Siwezi nikasema hivyo wakati haki zake zote za msingi alikuwa anapata, tofauti ni kwamba hatukuwa na mkataba naye. Funguka: Mbona kuondoka kwake kunafanana na uondokaji wa aliyekuwa mwanamuziki wako anayejulikana kwa jina la Venas au Anko Vena, hakuna kitu nyuma ya pazia? Asha Baraka: Hapana hakuna kitu chochote, ninavyojua Muumini anaenda kujiunga na bendi moja hivi, nasikia inaitwa Victoria Band na Anko Vena nimeambiwa amejiunga na bendi iliyo chini ya Jeshi la Polisi, ndiyo maana nakwambia hakuna kitu kama hicho. Endelea kufunguka hii ndio nafasi ya kutoa dukuduku lako. Asha Baraka: Kitu ambacho nampongeza Muumini ni pale aliponifuata na kuniambia ukweli kuwa anaondoka maana kuna sehemu amepata kazi. Nadhani kwake aliona kuna maslahi, hicho tu ndicho nampongeza kwani ameutendea haki ukongwe wake. Funguka: Mbona unasema unampongeza kwa kuja kukuaga, kwani wanamuziki wote walioondoka hawajawahi kukuaga? Asha Baraka: Chaz Baba aliniaga lakini kuna maneno alikuwa akiyazungumza sikuwa napendezwa nayo. Vena hakuniaga, nilishtukia tu hayupo ila Muumini alitumia busara sana kwani alijua haya ni maisha, kuna kupanda na kushuka na ndio maana alikuja kuniaga.Funguka: Ukiachana na ishu ya kuondoka kwa Muumini, mmejipanga vipi kuziba pengo la hao wanamuziki wawili walioondoka? Asha Baraka: Bendi kama bendi iko vizuri sana, hivi ninavyoongea na wewe jioni wanamuziki wote wanaingia studio kurekodi nyimbo mbili, ya Kalala na ‘J 4’, ndio maana nakwambia bendi iko vizuri we’ mwenyewe shahidi. Funguka: Kwa hiyo unataka kuniambia wapenzi wa Twanga Pepeta wategemee bonge la burudani Jumapili hii pale katika Ukumbi wa Dar Live Mbagala Zakhem jijini Dar? Asha Baraka: Siyo burudani tu ila kutakuwa na ‘surprise’ ya nguvu kutoka kwa wanamuziki wa Twanga, ninachowaomba wapenzi wa Twanga wafike kwa wingi Dar Live maana burudani waliyokuwa wakiikosa zamani pale Viwanja vya Sigara TCC sasa imehamia Dar Live. |
0 Comments