Maafisa wa polisi nchini Afrika kusini wameshutumiwa kuweka silaha karibu na miili ya wachimba migodi waliouawa karibu na mgodi wa palatinum wa Marikana.
Picha zilizowasilishwa mbele ya tume inayochunguza mauaji hayo zinaonekana kudhibitisha tuhuma hizi.
Picha moja inaonyesha mwili wa mwanamume aliyefariki katika sehemu iliyo karibu na mgodi wa Marikana.

Picha ya pili iliyopigwa baadaye lakini siku hiyo hiyo, ni sawa na picha ya kwanza lakini hii inaonyesha mwanamume yuyo huyo akiwa na panga lenye mkono wa rangi ya manjano lililo chini ya mkono wake wa kulia.


Picha zote zilipigwa na maafisa wa polisi wa Afrika kusini muda mfupi tu baada ya kuuawa kwa wachimba mgodi thelathini na wanne na polisi mnamo mwezi Agosti.

Kuna mifano zaidi.Hili lina maana kuwa eneo la tukio la uhalifu huenda lilibadilishwa na maafisa hao wa polisi ili kushinikiza kujitetea kwao kuwa waliwashambulia wachimba mgodi hao ili kujikinga.

Ushahidi unazuka katika tume inayochunguza mauaji hayo ya Marikana. Wakili George Bizos ambaye kwa wakati mmoja alimtetea Nelson Mandela, anasema kuna ushahidi mzito wa kujaribu kuzuia haki kutendeka.

Alitoa wito kwa maafisa wakuu wa polisi kueleza ni nini kilichofanyika.