Kufuatia ya moja kati ya mauaji makubwa kutokea katika historia ya Marekani, wanasiasa akiwemo Rais Barack Obama, wametaka sheria kuhusu umiliki wa bunduki nchini Marekani zibadilishwe, ili kuepusha maafa kama hayo siku za usoni. Akizungumza baada ya mauaji ya watoto na watu wazima 26 katika shule moja ya msingi katika jimbo la Connecticut Ijumaa, Rais Obama aliyeonekana kujawa na huzuni, alitoa wito kuchukuliwe hatua ya maana kuzuwia mauaji kwa kutumia bunduki.
Hakutoa maelezo zaidi.
Taarifa zaidi zimejitokeza kuhusu yaliyotokea katika mauaji hayo katika shule ya msingi ya Sandy Hook mjini Newtown.
Mshukiwa mwenye umri wa miaka 20 - aliyeitwa Adam Lanza - alimuuwa mama yake nyumbani kwake, kabla ya kuelekea katika shule hiyo na kuwafyatulia risasi wanafunzi.
Walioshuhudia walisema walisikia zaidi ya milio mia moja ya risasi na kuwaona watoto waliokuwa wakihofia maisha yao wakilikimbia jengo.
Wanafunzi hao walikuwa kati ya umri wa miaka mitano na kumi.
Wakaazi wa Newton wamekesha wakiomboleza.
Rais Obama ametoa amri kuwa bendera zipepee nusu mlingoti kwenye majengo ya taifa.
Akizungumza juu ya mauaji hayo, waziri mkuu wa Australia, Julia Gillard, alisema tukio hilo limezidi kusikitisha kwa vile waliouwawa ni watoto.