Mkuu wa Jeshi la Polisi Said Mwema .

WAKATI ujangili unaotishia kutoweka kwa baadhi ya wanyama katika hifadhi za taifa nchini ukiendelea kushika kasi, imebainika kuwa baadhi ya mahakimu, polisi na waendesha mashtaka ni wahusika wakuu wa matokeo ya ujangili ambao ni chimbuko la biashara ya nyara za Serikali zikiwamo pembe za ndovu.
Inakadiriwa kuwa tembo wapatao 30 huuawa kila mwezi na mtandao wa ujangili ambao pia unaundwa na wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ya nchi, ambao wamekuwa wakifanikisha uhalifu huo kwa msaada wa baadhi ya maofisa na askari wa wanyamapori.
Hapa nchini ujangili umekuwa ukifanywa na makundi ya watu wenye silaha haramu katika hifadhi za taifa, mapori ya akiba na maeneo mengine ya wazi, huku kukiwa na taarifa kwamba baadhi ya nyara hasa pembe za ndovu
huingizwa nchini kutoka nchi jirani ya Msumbiji. Wanunuzi wakuu wanadaiwa kuwapo hapa nchini.
Mkurugenzi wa Tanapa, Allan Kijazi anasema hali ni mbaya kwa kuwa taifa linatumia gharama kubwa kuwalinda na kukabiliana na ujangili, lakini wahalifu wanapokamatwa wamekuwa wakiachiwa kinyemela hata pale ambapo kuna ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani.
“Ujangili huu ni mtandao mkubwa sana. Wanatumia silaha za kisasa zaidi kuliko hata za kwetu…hata kibali cha kununua silaha hatupati kwa wakati, hali ambayo inadhoofisha jitihada hizi…hapa tulipofikia ushirikiano wa vyombo vyote ni muhimu,” alisema Kijazi.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa, njia kubwa ya kuingizia pembe hizo zipo katika wilaya za Tunduru, Namtumbo na Mbinga mkoani Ruvuma ambako pikipiki hutumika kuvusha kabla ya kusafirishwa kwa kificho hadi Dar es Salaam ambako hupakiwa kwenda nje ya nchi kuuzwa kupitia bandarini.
Kushamiri kwa vitendo vya ujangili kumesababisha kuwapo jitihada za kuukabili, lakini kama alivyosema Kijazi, imebainika kuwa jitihada hizo zinakwazwa na baadhi ya watumishi katika vyombo vya dola, wakiwamo baadhi ya mahakimu, polisi na waendesha mashtaka.
Uchunguzi wa Mwananchi ulibaini kuwa baadhi ya watuhumiwa ambao wamewahi kunaswa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ujangili, wametoweka katika njia za kutatanisha na kuacha kesi zikiendelea.
Mchezo mahakamani
Uchunguzi umebaini kuwa, baadhi ya mahakimu wa mahakama za wilaya katika mikoa ya Mara, Simiyu, Shinyanga na Kigoma ni sehemu ya mtandao huo, hivyo watuhumiwa wengi wanaokamatwa na nyara, zikiwamo silaha hupewa dhamana na hawarudi mahakamani.
Taarifa za uchunguzi zilizothibitishwa na baadhi ya maofisa wa Tanapa, askari wa wanyamapori na wanasheria wa Serikali zinadai kesi nyingi za nyara licha ya kuwa na uzito, baadhi ya mahakimu walioko chini ya mtandao huo hutoa dhamana kwa masharti nafuu na watuhumiwa huruka dhamana na kuendelea na kazi ya ujangili.
Uchunguzi umebaini mtuhumiwa aliyekamatwa kwa tuhuma za kuwinda faru, nyani na ngiri ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mwaka 2010, Madubu Masunga Dusara (33), mkazi wa Ng’walali, haonekani mahakamani baada ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Shinyanga, Lydia Ilunda kumpa dhamana kwa masharti nafuu.

CHANZO NI HAPA