Kikundi cha Jumuiya ya wanafunzi nchini India wakiwa wameshika mabango wakati wa maandamano ya kupinga vitendo vya ukatili likiwamo kitendo cha ubakaji kilichofanywa kwa mwanamke aliyefariki. Picha na AFP

NEW DELHI, India
MWILI wa mwanamke wa India ambaye amefariki hospitalini nchini Singapore baada ya kubakwa kinyama mjini New Delhi umerejeshwa nchini humo kwa ndege maalumu ya kukodi.
Balozi wa India nchini Singapore, T.C.A Raghavan aliwaambia waandishi wa habari jana, saa kadhaa baada ya mwanamke huyo kufariki kutokana na viungo vyake kushindwa kufanya kazi katika hospitali nchini Singapore ambako alikuwa akipatiwa matibabu.

Mwanamke huyo na ndugu wa marehemu walisafirishwa kwenda India katika ndege maalumu ya kukodi mchana wa jana Jumamosi, kwa mujibu wa Raghavan.
Waziri Mkuu wa India, Manmohan Singh alisema kuwa amesikitishwa sana na kifo cha mwanamke huyo ambaye alifanyiwa vitendo vya kinyama kwa kubakwa na kundi la vijana na kwamba maandamano yaliyozuka kutokana na kitendo hicho “yanaeleweka”.
“Nimesikitishwa mno kufahamu kuwa mwathirika huyo wa mashambulizi ya kinyama yaliyofanyika Desemba 16 mjini New Delhi ameshindwa kunusurika kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata baada ya shambulio dhidi yake, “ aliandika waziri huyo mkuu katika tovuti yake.
“Tumeshaona hisia na nguvu ambazo tukio hili limesababisha. Hii ni hali ambayo inaeleweka kutoka kwa vijana wa India ambao wanataka mabadiliko ya kweli.
“Nataka kuwaambia, familia yake na taifa kwa jumla kuwa amepoteza maisha, ni juu yetu wote kuhakikisha kuwa kifo chake hakitakuwa cha bure.”
India imetikiswa na maandamano makubwa tangu msichana huyo mwenye umri wa miaka 23 aliposhambuliwa kinyama katika basi mjini New Delhi na kundi la watu sita.
Serikali imekuwa ikijaribu kulituliza wimbi la hasira kwa kuahidi adhabu kali kwa uhalifu mkubwa unaohusiana na ngono pamoja na kuunda tume maalumu ya uchunguzi kuhusiana na jinsi ya kushughulikia kesi za ubakaji.
Wakati maofisa wakijitayarisha kwa ghasia zaidi mitaani, polisi waliongezwa katika eneo la kati la mji mkuu wa India kabla ya mwili wa msichana huyo kurejeshwa nchini humo jana.
Ofisa wa polisi wa mjini New Delhi, alihimiza watu kuomboleza kifo cha mwanamke huyo kwa amani wakati maeneo kadha ya mji huo mkuu yamefungwa.
Singh, ambaye hapo kabla alitoa wito wa utulivu , alisema kuwa itakuwa, “Heshima kubwa kwa kumbukumbu yake iwapo tutaweza kuelekeza hisia zetu hizi na nguvu katika kuchukua hatua sahihi. Kwa muda huu tunahitaji mjadala wa maana na uchunguzi kuhusiana na mabadiliko ya lazima na haraka ambayo yanahitajika katika mtazamo wa jamii.