Umoja Mataifa umesema helicopta kutoka kwa kikosi chake cha kutunza amani Sudan Kusini imeangusha na jeshi la nchi hiyo na kuwaua watu wanne waliokuwa ndani ya ndege hiyo.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema ndege hiyo ilishambulia wakati ilipokuwa katika harakati za kushika doria Mashariki mwa jimbo la Jonglei.
Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Eduado del Buey amesema jeshi la Sudan Kusini limekiri kushambulia helicopta hiyo.
Umoja wa mataifa umekuwa ukiwasaidia raia waliokwama ndani ya mapigano kati ya jamii mbili zinazozoana katika jimbo hilo la Jonglei.
''Ripoti za mwanzo zinaashiria kuwa ndege hiyo ya Umoja wa Mataifa ilianguka na kushinda moto. Kikosi chake kilianza haraka shughuli za kutafuta mabaki na manusura wa ndege hiyo. Hata hivyo imebainika kuwa watu wanne waliokuwa ndani ya ndege hiyo wameuawa'' msemaji huyo alisema.

Lakini katika mazungumzo kati ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wanaotunza amani nchini Sudan Kusini na jeshi la nchi hiyo SPLA, Umoja wa Mataifa umesema wanajeshi wa Sudan Kusini wamekiri walishambulia ndege hiyo katika eneo la Likuangole katika jimbo la Jonglei.
Waziri wa Habari wa Sudan Kusini, Barnaba Marial Benjamin, ameiambia BBC kuwa chanzo cha ajali hiyo hakijulikani.
Hata hivyo amekataa kuthibitisha au kukanusha kuhusika kwa wanajeshi wake.