Rais wa Malawi,Joyce Banda.

SIKU chache baada ya viongozi wa dini wa madhehebu ya Kikristo nchini Malawi na Tanzania kuwasiliana kwa lengo la kutaka wajadili mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa baina ya nchi hizo mbili, Serikali ya Tanzania imezuia mjadala huo, Mwananchi imeelezwa.

Viongozi hao wa dini, Baraza la Wakristo Tanzania (TCC) na Baraza la Wakristo Malawi (MCC) walitangaza kujiingiza kwenye mgogoro huo wakitaka washirikishwe kama wasuluhishaji katika kile walichoeleza kuwa mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu bila suluhu yoyote.
Hata hivyo Serikali ya Tanzania imepinga wazo la viongozi hao kwa maelezo kuwa suala la mzozo huo limefikishwa kwa mpatanishi maalumu ambaye amekubaliwa na pande zote mbili.

Hivi karibuni mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi zote mbili walikuwa mjini Maputo, Msumbiji kwa ajili ya kukutana na mpatanishi wa mzozo huo, Rais wa zamani Joachim Chissano ambaye anatazamia kuanza kazi hiyo Januari mwakani.


Kiongozi huyo wa zamani ndiye atayeongoza jopo la viongozi wastaafu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) kusaka suluhu ya mzozo huo ambao sasa umedumu kwa zaidi ya miongo 6.

Hata hivyo viongozi wastaafu wa Tanzania rais All Hassani Mwinyi, Benjamin Mkapa na yule wa Malawi Bakili Muluzi hawataruhusiwa kushiriki kwenye jopo hilo la marais wastaafu wa nchi za SADC.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amekaririwa akisema hoja iliyotolewa na viongozi wa dini waliotaka kuwa sehemu ya usuluhishi kwenye mzozo huo, haina nguvu kwani suala hilo limefikishwa kwenye ngazi ya juu zaidi.

Hivi karibuni Serikali ya Tanzania na Malawi zilipeleka barua ya pamoja kwa jukwaa la marais wa wastaafu wa nchi za kusini mwa Afrika linaloongozwa Rais Joachim Chissano, zikiomba zipatanishwe katika mzozo huo baada ya majadiliano ya pande zote mbili kushindwa kuzaa matunda. Hata hivyo duru za kidiplomasia kutoka Lilongwe zinasema kuwa, Serikali ya Malawi imejiandaa kuelekea kwenye Mahakama ya Haki ya Kimataifa(ICJ) iwapo upatanishi huo utashindwa kuzaa matunda.

Gazeti la Daily Times limewanukuu maofisa wa Serikali wakisema kuwa karata ya mwisho kwa Malawi itakuwa ni kuelekea kwenye mahakama hiyo ambayo pia imewahi kutoa ufumbuzi kwa mizozo mbalimbali iliyohusu mipaka.

Mahakama hiyo ya kimataifa imewahi kushughulikia mzozo wa mpaka uliozihusisha nchi za Cameroon na Nigeria zilizokuwa zikizozona kuhusiana na eneo lililojulikana Bakassi Peninsula.Kadhalika imewahi kutatua mzozo wa mpaka baina ya Namibia na Botswana kuhusiana na kisiwa Kasikil.