MVUA iliyoambatana na upepo mkali imebomoa nyumba 22 na kuacha wakazi wapatao 200 kukosa mahala pa kuishi.
Mbali na uharibifu huo, mvua hiyo pia imebomoa madarasa sita ya Shule ya Sekondari Mnacho iliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi na jengo la utawala la shule hiyo.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana, zimeeleza tukio hilo lililozua tafrani kwa wakazi wa eneo hilo, lilitokea juzi katika Kijiji cha Ngau Chimbira B, kilichoko halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa. “Uharibifu wote huo, ulitokea katika kipindi cha saa moja tu, ilipokuwa inanyesha mvua hiyo,” alisema mkazi wa eneo hilo Mwanaisha Seif.
Mkazi mwingine Issa Omari alisema mvua hiyo ilianza kunyesha saa 9:00 hadi 10:00 jioni ikiwa inaambatana na upepo mkali uliokuwa ikivuma kutoka Mashariki kwenda Magharibi.
Juma Said na Yohana Joseph, kwa nyakati tafauti wameeleza kwamba mvua hiyo iliyokuwa imeambatana na upepo mkali ilinyesha kwa takribani ya saa moja tu.
Diwani wa kata ya Ngau Chimbira, Beda Mbila alisema nyumba 28 zimeezuliwa mapaa na kimbunga hicho.
Diwani huyo alifafanua kuwa kutokana na tukio hilo waathirika wanahifadhiwa katika kwa ndugu na jamaa zao huku uongozi ukiendelea kuangalia namna ya kuwasaidia zaidi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Ruebern Mfune amekiri kupata kwa taarifa ya tukio hilo, na kueleza bado hasara iliyopatikana haijaweza kufahamika mara moja.
Mkuu wa wilaya ya Ruangwa Agnes Hokororo alisema ofisi yake imejipanga kushughulikia tatizo hilo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Kauli ya TMA Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya hewa nchini (TMA), Agnes Kijazi akizungumzia uharibifu huo alisema, hali hiyo ilitegemewa kwa kuwa utabiri uliotolewa na mamlaka hiyo Septemba mwaka huu, ulishaeleza hilo.
Kijazi alisema utabiri huo ulibainisha kuwa baadhi ya maeneo ya Kaskazini na Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, kutakuwa na upungufu mkubwa wa mvua na maeneo ya Nyanda za juu Kusini Magharibi katika mkoa ya Iringa, Mbeya na Rukwa na Kanda ya Ziwa yatakuwa na mvua nyingi zitakazoweza kusababisha uharibifu wa nyumba na mali.
|
0 Comments