Hata hivyo, Dk Slaa alipoulizwa iwapo ana nia ya kuwania nafasi hiyo alihoji: “Kwani mwaka 2010 nilijitangaza mwenyewe,? Iwapo wanachama wa Chadema watanipendekeza nitafikiria kufanya hivyo.” Mwasisi wa chama hicho Edwin Mtei, Wajumbe wa Kamati Kuu; Profesa Mwesiga Baregu na Dk Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa Bavicha John Heche na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema walitoa maoni yanayopingana kuhusu kauli hiyo ya Mbowe.
Wanaounga mkono
Mtei alisema anaunga mkono kauli ya Mbowe akisema kiongozi huyo hajakosea kumtangaza Dk Slaa kuwania urais mwaka 2015.
“Ninaunga mkono Dk Slaa kuwania tena nafasi ya urais mwaka 2015. Mwenyekiti amemtangaza baada ya kupata baraka ya vikao vya chama,” alisema Mtei.
Ingawa Mtei hakuwa tayari kusema ni kikao gani kilichopitisha jina la Dk Slaa kuwania nafasi hiyo, alisisitiza: “Kuna vikao vya Kamati Kuu vimefanyika hivi karibuni, vinaweza kuwa vimefanya uamuzi huo. Mwenyekiti hawezi kuzungumza jambo bila baraka za vikao vya chama.”
Hata hivyo, kauli hiyo ya Mtei inapingana na ile aliyoitoa Oktoba 6, mwaka huu baada ya Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kutangaza kutogombea tena ubunge badala yake kusema anataka kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Mtei alisema hatua ya Zitto kutangaza kuwania urais mapema kungesababisha mzozo na mpasuko ndani ya chama hicho.
Mtei alisema amekuwa akimshauri Zitto mara kwa mara kuhusu hatua yake hiyo akimtaka kuwaunganisha wana Chadema na siyo kuwagawa au kuwavuruga.
“Hakuna shida kuonyesha hisia, lakini unatengeneza mzozo mkubwa sana ukitangaza sasa. Mimi nimeshamshauri sana Zitto, ahakikishe anakiunganisha chama na siyo kukigawa wala kukivuruga.”
Alisema mbunge huyo kutangaza kutogombea tena ubunge na badala yake kujipanga kuwania urais mwaka 2015 kumekuja mapema mno na kuonya kuwa itaibua mzozo ndani ya Chadema.
Mtei ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, alisema kwamba wakati mwafaka ukiwadia, Chadema kitaamua ni nani mwenye sifa za kugombea urais huku akisema kina utaratibu wake wa kuwapata wagombea mbalimbali wa uongozi.
Hata hivyo, Zitto jana alikataa kuzungumzia suala hilo akisema: “Nimesikia hata mimi kwenye vyombo vya habari ila sina cha kuzungumza kuhusu hilo.”
Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche alisema kauli hiyo Mbowe siyo yake binafsi, bali ni ya wananchi.
0 Comments