Stori na Musa Mateja
MENGI waliyoyafanya mastaa kwenye msiba wa nyota wa Bongo Fleva na maigizo Bongo, Hussein Ramadhan Mkieti ‘Sharo Milionea’ yamejenga tafsiri ya aibu kwenye jamii ya wakazi wa Kijiji cha Lusanga, Muheza, Tanga.
Hayo yalijiri wakati mastaa hao ambao wengi ni wa filamu kufanya matukio yaliyowashangaza na kuzua minong’ono Wanakijiji wa Muheza.
Macho ya paparazi wetu yalibahatika kushuhudia baadhi ya wasanii waliofika msibani hapo wakienda kulala gesti jambo ambalo lilizua minong’ono kutoka kwa wenyeji wa Lusanga.
“Sasa hawa wanakwenda kulala wapi?” alihoji mzee mmoja, alipojibiwa gesti, akashutuka na kusema:
“Khaa! Mfano yule dada wa mbele si amelia sana hapa, mimi nilijua wana uchungu sana, watalala hapahapa na wafiwa kumbe sivyo.”
Kama vile hilo halitoshi, kuna mastaa maarufu sana ambao walilia mpaka kupoteza fahamu msibani, lakini baadaye waliondoka na kwenda hotelini ambako walijipodoa na kujiremba sana.
Aidha, baadhi ya mastaa siku walipofika Muheza, walikwenda kulala hotelini bila ya kufika msibani hadi kesho yake, tena wakati mwili wa marehmu ukipelekwa makaburini tayari kwa mazishi.
Minong’ono ilizidi nyumbani kwa wafiwa wakati zoezi la maziko likiendelea, kwamba baadhi ya wasanii ambao hawakulala msibani na kuchelewa kufika ndiyo waliolia zaidi, wengine walianguka na kupoteza fahamu.
Cha kushangaza sasa, baada ya mazishi mastaa hao walianza kupigana vijembe kupitia mitandao ya kijamii, wengi waliposti mada wakisema wengine wao ni wanafiki wakubwa kwa kuwa walijifanya kuguswa na kifo cha Sharo Milionea lakini walirudi Dar es Salaam dakika chache tu baada ya kumaliza mazishi.
Ray, yeye aliwashangaza zaidi watu wa Lusanga kwa kutinga msibani akiwa amevaa ‘singilendi’ ambapo alipitiliza hadi kwa mama wa marehemu kumpa pole.
Malezo ya wakazi wa Lusanga yalikuwa haya: “Leo tumejionea mengi kutoka kwa watu wanaojiita maarufu, yaani wanakuja msibani wamepaka poda utafikiri wauza sura, wengine wana kope ndefu kama kinga za mabomu ya machozi loh! Hiyo ni elimu tosha kwetu.”
Mila na desturi za wenyeji wa Wilaya ya Muheza ambao wengi ni wa kabila la Kibondei, mtu anapokuwa msibani anatakiwa kuachana na tabia zenye kuashiria anasa, kama vile kulala kwenye vitanda au kuoga na kubadili nguo kabla ya siku ya tatu ya msiba.
Wasanii waliotia fora kwa kuonesha adabu na umakini ni Adamu Kuambiana, Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba na William Mtitu.