Kumetolewa wito wa kimataifa kwa wakuu wa Algeria wafanye kila wawezalo kuhakikisha usalama wa mateka ambao bado wanazuwiliwa na wapiganaji wa Kiislamu kwenye kinu cha gesi katika jangwa la Sahara.Siku tatu baada ya watu waliokuwa na silaha kem-kem kuanza kushambulia kinu hicho, serikali za Japani na Marekani ni kati ya zile zilizoisihi Algeria kuhakikisha kuwa usalama wa mateka hao ndio jambo muhimu kabisa.
Shirika la habari la taifa la Algeria linasema sasa inajulikana mateka kama 12, wageni pamoja na wananchi, wameuwawa katika kinu cha gesi baada ya wapiganaji wa Kisslamu kushambulia kinu hicho na kuwateka wafanyakazi siku ya Jumatano.

Ripoti ya Algeria piya ilisema kuwa wapiganaji kama 18 waliuwawa na wageni kama 30 wametoweka.
Lakini ilisema watu 100 walikombolewa.
Shirika la habari la Algeria lilieleza kuwa wapiganaji 30 kutoka nchi mbali-mbali walishiriki kwenye shambulio hilo.
Inaarifiwa kuwa askari wa Algeria bado wanawasaka wapiganaji au mateka ndani ya kinu hicho.
Waziri wa habari wa Algeria, Mohand Belaid Oussaid, ametetea hatua zilizochukuliwa na serikali katika msukosuko huo.
Alisema ilibidi wachukue hatua haraka:
Hawa wafanyakazi kutoka ng'ambo ni wageni wa Algeria, ina jukumu juu yao, na hatuwezi kukubali shambulio kama hilo la kihalifu.
Ndio sababu hatimae wakuu wa jeshi walipokuwa na hakika kuwa hawana wakati, ilibidi tuchukue hatua haraka.
Ingekuwa hatukufanya kitu, wangeweza kuwauwa mateka.
Kwa sababu wapiganaji walikuwa wamevinjari kwamba hawataondoka.
Ndio sababu ilibidi tufanye haraka na haya ndio yaliyotokea.
Matokeo kwa sasa naona kwamba tumeepusha janga kubwa, mauaji makubwa.