Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS), Dk. Efesper Nkya,
amesema wastani wa chupa za damu 250,000 zinahitajika kwa mwaka kusaidia
mahitaji ya damu kwa wajawazito na watoto.
Wakati kiasi hicho kikilenga kundi hilo mahitaji ya damu kitaifa ni wastani wa chupa 400,000 kwa mwaka.
Alikuwa akizungumza kwenye kampeni maalum ya uzinduzi wa kuhamasisha
watu kutoa damu inayoitwa Mamaye, iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa
la Evidence for Action iliyofanyika jijini hapa jana.
Dk. Nkya aliwataka Watanzania kujenga tabia ya kutoa damu kwa hiari ili kuwasaidia wenye shida hususan, wanawake na watoto.
Alisema licha ya taifa kuhitaji chupa 400,000 ni wastani wa chupa
120,000 hadi 150,000 zinazopatikana kwa mwaka na kwamba haitoshelezi
mahitaji ya nchi.
Zoezi la kutoa damu kwa hiari ni sehemu ya juhudi za serikali
kuhakikisha kuwepo kwa akiba ya damu kwa ajili ya watu wenye shida
ambao wengi ni wajawazito na watoto wa chini ya miaka mitano.
“Watoto walio chini ya miaka mitano wamo katika hatari kubwa ya kupata
magonjwa ya malaria na hatimaye wanahitaji kuongezewa damu. Kwa hivyo,
utoaji wa damu wa hiari ni muhimu .
“Kama asilimia moja ya Watanzania wanaweza kutoa damu kwa kila mwaka, Tanzania haitakuwa na upungufu wa damu,” alisema.
Alisema zoezi hilo lililoanza Jumapili iliyopita, limekusanya zaidi ya
chupa 700 za damu na kukaribia kufikia malengo ambayo ni chupa 1000 za
damu.
Mkurugenzi Mkazi wa Evidence for Action (E4A), Tanzania, Craig Ferla,
alisema wanawake wajawazito 8,000 wanakufa wakati wa kujifungua na
watoto 50,000 wa chini ya miaka mitano na wale wanaozaliwa wanapoteza
maisha kila mwaka kwa sababu upungufu wa damu.
E4A inaweka mkazo katika kuboresha maisha na kuhamasisha uwajibikaji ili
kulinda maisha ya wajawazito na watoto wanaozaliwa. Pamoja na Tanzania,
nchini zingine ambazo zimo kwenye mpango huo ni Ethiopia, Ghana,
Malawi, Nigeria na Sierra Leone.
“Hii ni hatua kubwa lakini tunahitaji kufanya kitu zaidi ya hatua hii,”
alisema na kuongeza, “kwa lugha ya kawaida, inamaanisha kwamba kila siku
wanawake 20 na karibu watoto 139 wanafariki kutokana na matatizo ya
uzazi.”
Aliongeza, “tunahitaji kuchukua hatua zaidi kupunguza hii idadi kubwa ya
wanawake na watoto wanaofariki kwa sababu tu ya kukosa damu.”
Alisema ni suala la kibinadamu kujitolea kutoa damu kwa mahitaji ya
jamii na kwamba huo ni wajibu wao kuhakikisha kundi hilo la wanawane na
watoto linaokolewa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Jowika Kasunga, ambaye
alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa
Mulongo, alikemea tabia ya baadhi ya hospitali, vituo vya afya na
zahanati kuuza damu kwa wagonjwa.
Alisema damu zinazotolewa hazipaswi kuuzwa na kwa wale wanaofanya hivyo
ni lazima wachuliwe hatua kali za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi.
Aliwataka wananchi kuwafichua wafanyakazi wa sekta ya afya wanaojihushisha na biashara ya kuuza damu kwa wagonjwa.
|
0 Comments