Wanachama wa CCM katika moja ya mikutano.

CHAMA Cha Mapinduzi katika Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga kimefanya mabadiliko kwa kuwaondoa wapangaji wote waliokuwa wamepanga bila kulipa kodi ya pango na wengine kukaa bure kwenye vibanda vyake vya biashara vilivyopo Kahama.
Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama, Michael Bundalla alisema mabadiliko hayo makubwa yamefanywa na kamati ya siasa ya wilaya, baada ya kuunda kamati ya wajumbe watatu ya kupitia upya mikataba ya wapangaji hao.
Bundalla alisema katika kupitia upya mikataba hiyo, kamati ilibaini baadhi yao wamejipachika kwenye  vibanda ambapo si wapangaji halali wanaotambuliwa na chama, ambapo kamati ya siasa imewapa siku saba wawe wameishaondoka kwenye majengo hayo.
Aidha Bundalla alisema tatizo jingine lililojitokeza ni waliokuwa wapangaji kupangisha wengine kwa bei kubwa, huku kwenye chama wakilipa fedha kidogo hali ambayo amedai ni ukiukwaji wa mkataba unaoelekeza kutopangisha mwingine.
Kutokana na hali hiyo, kamati ya siasa katika kikao cha kupitia maombi mapya ya wapangaji hao iliwaondoa wote waliobainika kukiuka mikataba hiyo ikiwa ni pamoja na wale waliovifanyia marekebisho ya kuvigawa mara mbili bila ya idhini ya Chama Cha Mapinduzi ambacho ndicho mmiliki wa vibanda hivyo. Kwa upande wake,  Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kahama,  Mabala Mlolwa alisema uamuzi wa kuweka mikakati hiyo ni kukifanya chama kijiimarishe kiuchumi na kuwataka wanaolalamika kuacha kupoteza muda wao kwani kamati yake haitatengua uamuzi wa kuwaondoa kwenye vibanda hivyo.
Kauli hiyo imekuja baada ya baadhi ya walioondolewa kwenye vibanda hivyo kulalamika kwenye vyombo vya habari kuwa hawakutendewa haki,  hali ambayo Mwenyekiti huyo alisema kamati yake iliwaondoa wale wakorofi waliokuwa wakifanya shughuli  zao bure kwenye vibanda hivyo na wale ambao walikuwa wamejipachika  kwenye maeneo ya watu wengine.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete aliwatangazia viongozi wote wa chama hicho kujiimarisha kiuchumi kwa kuimarisha vyanzo vya mapato, ili waachane na kuchangisha wananchi wakati wa utekelezaji wa shughuli za kichama hali ambayo Kahama wameanza kwa kuondoa wapangaji wao wanaokwepa kulipa.
Katika mpango huo, CCM Wilaya ya Kahama itakuwa na uwezo wa kukusanya zaidi ya Sh5 milioni kila mwezi kutoka vyanzo vyake vya mapato kupitia vibanda hivyo, ambavyo awali vilikuwa haviingizi mapato ipasavyo kutokana  na  wapangaji hao  kuwa wakorofi wakati wa malipo.