SERIKALI ya Uswisi imesema Serikali Tanzania haijaonyesha nia ya dhati kutaka kuchunguza na kupata mabilioni ya fedha yaliyofichwa na Watanzania katika benki mbalimbali nchini humo.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumamosi, jijini Dar es Salaam jana, Balozi wa Uswisi nchini, Olivier Chave alisema mpaka sasa hakuna jitihada zozote zilizofanywa na Serikali ya Tanzania kutaka ufumbuzi wa tuhuma hizo.

Balozi Chave alisema hayo muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo yake ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe. Hata hivyo wote wawili hawakuwa tayari kueleza ni kipi kilichojiri katika mazungumzo yao.Katika kikao cha tisa cha Bunge, Novemba mwaka jana, Zitto aliwasilisha hoja binafsi kulitaka Bunge kuchunguza na kuielekeza Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha na mali haramu nje ya nchi.



Katika mazungumzo yake jana, Chave alisema: “Uswisi iko tayari kushirikiana na Tanzania kujua uhalali wa fedha hizo na endapo zikigundulika ni fedha chafu basi tutazirejesha nchini.” Aliongeza:
“Serikali ya Uswisi haina tatizo kwani tumeshafanya hivyo kwa nchi za Ufilipino na Nigeria hivyo tutafurahi na Tanzania kama tutamaliza suala hili”. Alisema habari zinazoandikwa kuhusu mabilioni hayo kuhifadhiwa katika Benki za Uswisi, zinaharibu picha ya nchi hiyo mbele ya mataifa mengine, hivyo angependa suala hilo kumalizwa na kwamba wao wako tayari kusaidia.

Kauli ya Zitto
Kwa upande wake, Zitto alisema hadi sasa Serikali haijamfuata kutaka kutoa ushirikiano wa aina yoyote kuhusu tuhuma hizo.
Alisema kuwa ingawa Serikali ilitaka iachiwe tuhuma hizo ili iweze kuzifanyia kazi, lakini hadi sasa ukimya umetawala.

“Tangu kuahirishwa kwa kikao cha Bunge sijafuatwa na AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) wala mtu yeyote na sijui kipi kinachoendelea,” alisema Zitto na kuongeza:

“Nitaandika barua na kumkabidhi AG siku ya Jumatatu (keshokutwa ), nitahoji nini kinachoendelea katika uchunguzi huo.”

Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Naibu Katibu Mkuu Chadema, alisema Serikali ya Tanzania haionyeshi nia ya kuzihitaji fedha hizo. Aliongeza kwamba kuna njia mbili za kuwabaini walioficha mabilioni hayo nchini Uswisi. Kwanza ni kwa Serikali ya Tanzania kushirikiana na Serikali ya Uswisi, pili ni ulipaji wa kodi wa fedha ambazo Watanzania wameweka katika benki nchini humo.

“Njia hii ya pili nayo ni rahisi kwa sababu ukienda kuuliza Uswisi wanaolipia fedha hizo utapata majina yao. Hivyo Serikali itaweza kukamilisha taarifa yake na kuiwasilisha bungeni katika kikao kijacho” alisema Zitto.

Taarifa kutoka Benki Kuu ya Uswisi inaonyesha kuwa baadhi ya fedha hizo zimewekwa katika akaunti za vigogo hao na kampuni za mafuta na gesi zilizopo nchini.