NINAJIBU tahariri ya gazeti hili, toleo la Jumanne, Januari 15, 2013 iliyokuwa na kichwa cha habari, ‘Kiingereza sasa ndiyo lugha ya dunia’  
Tahariri hiyo ililenga kupinga hoja zilizotolewa na Mamlaka za Elimu Tanzania ambazo zote kwa pamoja zilipendekeza hivi karibuni kuwa Kiswahili iwe ndiyo lugha ya kufundishia kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu.
Mamlaka hizo ni Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Baraza la Mitihani (NECTA), Tume ya Taifa ya Sayansi (COSTECH), Baraza la Taifa la Ufundi (NACTE),  Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA).
Kwa hakika mamlaka hizi zinastahili pongezi kwa kutoa maoni hayo kwani yamegusa panapotakiwa.


Katika tahariri yenu mlitoa hoja mbalimbali kuhusiana na mapendekezo hayo ya mamlaka za elimu mkionyesha kuwa kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia kutaiondoa Tanzania katika ramani ya dunia jamani!
Wahenga husema mkataa kwao ni mtumwa! Labda kwa nafasi hii ndogo nijibu hoja zenu na niwaongezee hoja zaidi ili muweze kuwa wazalendo na kuelewa kwa nini wadau wa Kiswahili tunadai haya.
Mamlaka hizi zimezingatia mahitaji ya wateja wao, ambao ni watahiniwa, wanafunzi Watanzania wa ngazi mbalimbali za elimu ambao mamlaka zimegundua kuwa kuendelea kutumia Kiingereza ni kushusha kiwango cha elimu nchini, huo ni ukweli usiopingika.
Mimi kama mwalimu wa sekondari na hata vyuo naamini kuwa mwanafunzi katika somo la Uraia (Civics) anaulizwa kwa Kiingereza kutaja rangi zilizopo kwenye bendera ya taifa lake aelezee zina maana gani, haieleweki.
Wanafunzi wetu wanashindwa kueleza hayo kwa Kiingereza.  Je, vipi swali kama hilo mwanafunzi angetahiniwa kwa Kiswahili, angeshindwa?  Kujua elimu hii ya uraia ni suala la dunia au ni letu?
Ni vyema mkatambua kuwa maarifa na lugha ni vitu viwili tofauti.  Mtu anaposomeshwa Jiografia, Historia, Fizikia n.k. lengo ni kupata maarifa hayo, ili yaweze kumnufaisha yeye na jamii yake, kama ilivyo kwa waandishi wa habari wenye taaluma ya habari, mnatupatia elimu na kutuhabarisha Watanzania kwa Kiswahili, ingawa huenda mlisomeshwa kwa Kiingereza.
Lakini, mkitumia Kiingereza ni Watanzania wangapi wangejua mnachotuhabarisha? je, nyie waandishi ni wangapi wanaoweza kuandika Kiingereza fasaha na sanifu?  Je, mauzo ya gazeti lenu la Kiingereza na ya Kiswahili yapo sawa?  
‘Kiingereza ni cha dunia, Kiswahili ni cha kwetu’, mlisomeshwa kwa Kiingereza mnatuhabarisha kwa Kiswahili kwa faida ipi?  Ni bora mkasomeshwa kwa Kiswahili na pengine maarifa yenu yangekuwa makubwa mno, mngetunufaisha na elimu yenu.
Hakuna mgonjwa atakayekwenda hospitali akatibiwa kwa Kiingereza. Hakika atatibiwa kwa lugha anayoielewa na maarifa ya daktari wake hata kama kayapata kwa lugha ya Kirusi, Kijapani ai Kiarabu, lakini akimhudumia Mswahili atapona. Barabara nzuri na majengo mengine yanajengwa na Wachina, Wakorea ni maarifa waliyonayo na si lugha?