RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein ametakiwa kuchukua hatua
madhubuti za kuwawajibisha watendaji wa Serikali wenye kufanya
ubadhirifu wa fedha na kuisababisha Serikali hasara.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti
Hesabu za Serikali na Mashirika, Baraza la Wawakilishi, Omar Ali Shehe
alitoa ushauri huo wakati akifanya majumuisho ya maoni na michango ya
wajumbe wa baraza hilo yaliyotolewa wakati wa kuchangia ripoti ya kamati
hiyo.
Shehe alisema, Dk Shein anatakiwa kuwa jasiri na
kujiamini katika uchukuaji wa hatua kama anavyofanya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ambaye amewawajibisha viongozi
mbalimbali wakiwemo mawaziri kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa fedha
serikalini. “Bahati nzuri Mheshimiwa Kikwete anafuata sera za Chama
Cha Mapinduzi na Dk Shein pia anafuata sera na kanuni za chama hicho kwa
hivyo namwomba sana Dk Shein afuate na aige mfano anaouchukua Mwenyekiti wake,” alisema.
Wakitoa maoni yao wawakilishi walitaka Serikali
kuchukua hatua kutokana na fedha nyingi za Serikali kupotea bila ya
wahusika kuchukuliwa hatua licha ya ripoti hizo kutoa mapendekezo
kadhaa.
Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni, Mahmoud Mussa
Abdallah (CCM), alisema anakubaliana na ripoti hiyo iliyowasilishwa
lakini bado kunahitajika kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wahusika na
kuona vyombo vya sheria vitakavyolishughulikia suala hilo kuwa makini
katika kuifanyia kazi ripoti hiyo.
Alisema Zanzibar inafuata utawala bora na
haitakuwa busara kuona kazi kubwa iliyofanywa na kamati hiyo ikaachwa
bila ya kuchukuliwa hatua kwa watendaji waliotajwa katika ripoti hiyo.
Mwakilishi huyo alisema ni kweli ndani ya Shirika
la Umeme Zanzibar kumekuwa na matatizo na waliofanya hivyo hawakutumwa
na vyama vyao kwani ndani ya CCM inakataza wala rushwa na wezi na ni
vyema Serikali ikawachukulia hatua za kisheria wahusika wote. Mwakilishi
wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF), Ismail Jussa Ladhu, alisema Serikali
bado haijaonyesha umakini na hivyo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wana
haki ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Serikali kutokana na
kutokuwana hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika wa ubadhirifu wa
mabillioni ya fedha.
Alisema wajumbe wa baraza hilo waone kuwa,
wanaendelea kufanya kazi ya kuwatumikia zaidi wananchi kwa kuelezea
mambo wanayoyataka yakiwemo kufichua mambo maovu yanayotokea.
Jussa alisema wakuu wa Shirika la Umeme Zanzibar
(ZECO) wapo wenye kutumia huduma ya umeme bila ya kulipia jambo ambalo
gharama zao hulipishwa wananchi wanyonge. Hiyo inaweza kuwa ni hatari
kwa taifa huku akitahadharisha kuwepo kwa matabaka. Kwa upande wake
Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, Salmin Awadh Salmin (CCM), akitoa
maelezo yake alisema anasikitishwa na Ofisi ya Mdhibiti wa Serikali
kuona imeshindwa kubaini ubadhirifu huo uliotokea katika shirika hilo.
|
0 Comments