MASHEIKH wawili ambao ni viongozi wa Jumuiya ya Uamsho ya Zanzibar, wameongezwa katika kesi ya kuhatarisha  usalama wa nchi na hivyo kufanya idadi ya washtakiwa katika kesi hiyo kufikia kumi.
Walioongezwa katika kesi hiyo jana katika Mahakama ya Mkoa Vuga mjini Unguja  ni Abdallah Said Ali (48) ambaye ni Katibu wa Jumuiya ya Uamsho na Fikirini Majaliwa Fikirini (48) ambaye ni Mhadhiri wa Jumuiya hiyo.
Walisomewa mashtaka ya kufanya hujuma kwa kutoa maneno ya uchochezi katika mihadhara mbalimbali katika maeneo ya mji wa Unguja katika Mei 26 na  Oktoba 19 mwaka jana.
Pia wanadaiwa kuwachochea wananchi kuvunja amani na kuharibu mali zilizogharimu Sh 500 milioni.
Viongozi wa Uamsho wakipelekwa mahakamani.

Akisikiliza kesi hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Mkoa, Yessaya Kayange, alikataa kutoa dhamana kwa washtakiwa kwa maelezo kuwa kuna hati ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) inayozuia washtakiwa hao kupewa dhamana.
Kuhusu ombi la washtakiwa la kutaka kesi yao isikilizwe katika Mahakama Kuu, hakimu  alisema ombi hilo tayari limeshapelekwa na linasubiri majibu.
Wakili wa upande wa utetezi, Abdallah Juma, alidai kuwa washtakiwa hawapaswi kushtakiwa kwa sheria ya Usalama wa Taifa.

“Wateja wangu wamefungwa midomo katika mahakama hii. Kila siku wanaletwa hapa na hawatakiwi kusema chochote, kwa hiyo naomba wapelekwe Mahakama Kuu mbele ya Jaji ili waweze kupewa haki ya kusema kwani huenda wenyewe wakakiri makosa yao,” alidai Wakili Juma.
Wakili Juma alidai kwa sababu Mahakama ya Mkoa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, basi haina haki pia ya kuwapeleka rumande na kuwataka wateja wake waachiwe na kurudi nyumbani.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Rashid Abdallah na Raya Mselem, walikataa madai ya wakili wa utetezi wa kutaka kesi hiyo kusoma upya kwa sababu kuna washtakiwa wawili wameongezwa.
Hata hivyo walisema  hawana pingamizi na  dhamana lakini waendelee kushtakiwa kwa sheria ya Usalama wa Taifa.
Kesi hiyo inasikilizwa chini ya ulinzi mkali wa  polisi.
Washitakiwa wa awali katika kesi hiyo ni, Masheikh Farid Hadi Ahmed (41), Mselem Ali Mselem (52), Mussa Juma Issa (37), Azzan Khalid Hamdan (48), Suleiman Juma Suleiman (66), Khamis Ali Suleiman (59), Hassan bakar Suleiman (39) na Gharib Ahmad Omar (39).
Kesi hiyo itatajwa tena Januari 14 mwaka huu.