Serikali ya Uingereza inatarajiwa kujadili mpango wa kutoa msaada zaidi kwa wanajeshi wa Ufaransa wanaopambana na waasi nchini Mali.
Waziri mkuu David Cameron, amesema kuwa huenda msaada za usafiri na kijasusi ukatolewa kwa wanajeshi hao. Ndege mbili za kijeshi tayari zimetolewa kwa jeshi la Ufaransa.

Wanajeshi wa Mali wampokea msaada kutoka kwa Ufaransa na sasa Uingereza inataka pia kuwasaidia.

Waziri wa ulinzi anasema kuwa hakuna mipango ya kufanya mashambuli ya ardhini kwa sasa.
Kuhusu vifo vya raia wa Uingereza katika mashambulizi kwenye kiwanda cha gesi nchini Algeria yaliyofanywa na wapiganaji wa kiisilamu, bwana Cameron alisema kuwa eneo la Kaskazini mwa Afrika linageuka kuwa ngome ya wapiganaji wa kiisilamu.

Wasiwasi kuhusu athari za kundi la kigaidi la al-Qaeda katika ukanda huo, zinaonekana kudhibitiwa kufuatia mpango wa kuwapeleka wanajeshi wa Ufaransa kupambana na wapiganai wenye uhusiano na Al Qaeeda nchini Mali na Algeria ambako waliwateka nyara wafanyakazi wa kigeni.
Wanamgambo waliowashambulia wafanyakazi wa kigeni nchini Algeria, ambapo takriban mateka 48 waliuawa wametoa wito kwa Ufaransa kusitisha harakati zao nchini Mali.

''magaidi kuhangaishwa''

Waiziri mkuu alisema kuwa Uingereza pamoja na washirika wake wako katika mapambano dhidi ya kasumba ambayo inatia doa kubwa dini ya kiisilamu na ambayo inaamini kuwa mauaji na ugaidi yanakubalika na tena ni sharti yafanyike.
Jibu la jamii ya kimataifa kwa tisho hili liitakuwa swala muhimu katika ajenda ya mkutano wa nchi nane zilizostawi duniani G8.
"lazima tupambane na hao magaidi kwa kutumia mbinu zote za kuweka usalama. Lazima tuwakomeshe, kijeshi. Ni lazima tuzungumzie hii kasumba yao, sharti tufunge hii nafasi wanayoitumia, kuendesha harakati,zao'' alisema waziri mkuu.