Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani  

WAKAZI wawili wa Kijiji cha Karungu, Kata ya Ivuna, Wilaya ya Momba, mkoani Mbeya wamefariki dunia baada ya kufukiwa wakiwa hai katika kaburi moja na marehemu wanaodaiwa kumuua, tukio linalohusishwa na imani za kishirikina.

Watu hao, Ernest Molela anayekadiriwa kuwa na umri zaidi ya miaka 60 na Bibi Mizinala Nachela ambaye umri wake unakadiriwa kuwa zaidi ya miaka 50, walizikwa wakiwa hai pamoja na aliyekuwa mkazi wa kijiji hicho, marehemu Nongwa Hussein.

Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ivuna, Joseph Silwimba aliliambia gazeti hili jana kwa simu kuwa, tukio hilo lilitokea juzi kati ya saa tano na sita mchana, muda mfupi kabla ya maziko ya Hussein.Kabla ya kufukiwa katika kaburi moja na marehemu, Molela na Nachela kwa nyakati tofauti walipigwa hadi kuzirai na watu wanaodaiwa kushiriki kuchimba kaburi kwa ajili ya kumzika marehemu Hussein.



Silwimba alisema Hussein alifariki dunia Jumamosi saa 10 jioni baada ya kuugua kwa muda mrefu, lakini inaonekana kuwa baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walihusisha ugonjwa huo ambao ulisababisha kifo chake na ushirikina.

Jana mchana, Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Momba aliyefahamika kwa jina la Wendo aliongoza operesheni ya kufukua kaburi walimozikwa watu hao, ambao walikutwa wakiwa wameshafariki dunia.

Silwimba alisema miili ya Molela na Nachela ilifanyiwa uchunguzi, kisha kukabidhiwa kwa ndugu na jamaa zao ambao waliifanyia mazishi jana mchana.

Mkasa wenyewe
Kundi la vijana tisa ambao wanadaiwa kuwa ndiyo waliokuwa wakichimba kaburi la marehemu Hussein walianza msako katika Kijiji cha Karungu wakiwatafuta wale waliowatuhumu kwamba ni wachawi na kwamba walihusika na kifo chake.

Silwimba alisema katika harakati zao, walikwenda nyumbani kwa George Hussein ambaye ni kaka wa marehemu lakini hawakumkuta, hivyo kuamua kuchoma moto nyumba yake kwa kuwa walikuwa wakimtuhumu kuhusika na kifo hicho.

“Baada ya kufanya uharibifu huo, walikwenda hadi nyumbani kwa Mzee Molela kisha wakamkamata na kumpiga sana hadi hali yake ikawa mbaya kisha wakambeba hadi eneo la maziko,” alisema na kuongeza:

“Waliporejea kwenye msiba walimkuta Mama Nachela naye wakamkamata na kuanza kumpiga hadi akazimia na yeye pamoja na Molela waliwavuta hadi kwenye kaburi ambako mazishi ya Nongwa (Hussein) yalifanyika.”

Alisema baada ya jeneza kushushwa kaburini, vijana hao wanaodaiwa kwamba walikuwa na hasira walimvuta Molela na kumwamuru kuweka udongo kaburini, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na hali yake kuwa mbaya.

“Baada ya kushindwa walimsukumiza kaburini na baadaye walimvuta yule mama (Nachela) ambaye naye alikuwa hajitambui na kumtupa ndani ya kaburi halafu wakawafukia wote, kisha wakaondoka,” alisema Kaimu Ofisa Mtendaji huyo.