MWENYEKITI wa NCCR Mageuzi, James Mbatia jana alijikuta katika
wakati mgumu baada ya kulazimika kufungiwa katika ofisi ya NCCR-Mageuzi
wilaya ya Mtwara Mjini kutokana na baadhi wa wananchi walioudhuria
mkutano wake wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mashujaa, kutaka kumdhuru
kwa madai kwamba hawakuridhishwa na hotuba yake.
Mbatia alianza kurushiwa chupa tupu za maji
alipokuwa akitoka uwanjani hapo baada ya kukatisha hotuba yake kutokana
na baadhi ya wananchi kupinga kauli zake kwa madai hawamuelewi.
Kauli inayodaiwa kumgharimu Mbatia ni ile ya
‘Iwapo gesi itatoka Mtwara’ ndipo wananchi hao walipoanza kupaza sauti
wakisema “Hatukuelewi…hatukuelewi” hata hivyo Mbatia aliendelea
kuhutubia hali iliyosababisha wananchi hao wapaze sautzao kwa kuimba nyimbo.
“Haitoki… Hatoki…Haitoki…” sauti za wananchi
zilisikika na hata Mbatia alipojaribu kuwatuliza wananchi hao kwa kusema
‘gesi kwanza…. Gesi kwanza” baadhi waliitikia na wengine waliendelea
kusema hawamuelewi.
Hali hiyo ilimlazimisha Mbatia kukatisha hotuba
yake saa 11.25 jioni na aliondoka uwanjani hapo kwa kutembea kwa miguu
hali iliyotoa mwanya kwa wananchi kumrushia chupa tupu za maji.
Mwenyekiti huyo akiwa ameambatana na wabunge wa chama hicho, Moses
Machali (Kasulu Mjini) na Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini) mkoani
Kigoma, walielekea kituo cha polisi kilichopi karibu na uwanja huo na
baadaye alielekea ofisi za NCCR Mageuzi wilaya.
Alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo, Mbatia
hakupatikana kupitia simu zake zote za mkononi hata wabunge Buyogela na
Machali pia simu zao zilikuwa zimefungwa.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, Mary Nzuki
alisema hakuwa na taarifa za Mbatia kunusurika kupigwa ila aliahidi
kufuatilia suala hilo. “Ninachojua Mbatia yuko hapa kweli na amefanya
mkutano wake, baada ya mkutano ule akiwa anatoka eneo la mkutano alikuwa
anasindikizwa na wafuasi wake ambao walikuwa wanamshangilia. Sasa kama
walipofika huko mbele walimgeuka hilo sijui”, alisema Nzuki.
Pinda afunguka
Wakati huohuo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
amewasihi wakazi wa mikoa ya Kusini kuwa wavumilivu na kuruhusu mradi wa
kusafirisha gesi kutoka mikoa hiyo kwenda Dar es Salaam ufanikiwe kwa
kuwa una faida kubwa kwao.
Pinda alitaja manufaa hayo kuwa ni pamoja na ajira
kwa vijana watakaoshiriki katika ujenzi huo, ujenzi wa viwanda na
miundombinu na upanuzi wa Bandari ya Mtwara.
“Nilishangaa kuona wananchi wa Mtwara wanaandamana
kupinga ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka huko kwenda Dar es
Salaam. Mradi huo ndiyo utakuwa suluhisho la tatizo la umeme nchini,
”alisema Pinda na kuongeza:
“Wananchi wa Mtwara wawe wavumilivu, watanufaika
sana na mradi huo. Mradi utajumuisha upanuzi wa Bandari ya Mtwara pamoja
na ujenzi wa Viwanda mbalimbali vitakavyosaidia kukuza uchumi wa maeneo
yao kwa kutoa ajira na kukuza biashara zao.”
0 Comments