KILA mtu ana staili yake katika kufanya kazi inayomuingizia kipato, wapo wasanii wa filamu wanaofanya kazi zao waziwazi na wengine hupenda kujificha.
Amani linashuka na listi ya wasanii ambao wapo ndani ya gemu kitambo lakini staili yao si ya ‘kuanika’ sana kazi zao.
   
JACOB STEVEN JB: Anapiga mzigo chini ya kampuni yake ya Jerusalemu Film Company. Staili yake ya maisha unaweza kusema hayupo vile, asikwambie mtu jamaa anapiga mzigo, anakubalika na aliwahi kushinda tuzo za Ziff katika kipengele cha Msanii Bora wa Kiume mwaka 2011.

ISSA MUSSA ‘CLOUD 112’ Ni miongoni mwa wasanii ambao mara nyingi hawapendi kujionesha katika vyombo vya habari. Filamu zake ni nyingi na mafanikio yake ni makubwa, zinapendwa na watu wengi.

RUTH SUKA ‘MAINDA’ Mainda ni zao la Kundi la Maigizo la Kaole, mara nyingi huwa haonekani. Anapenda kufanya mambo yake kwa vitendo bila mbwembwe. Filamu zake ni nzuri, ana uwezo mkubwa wa kuigiza.

BLANDINA CHAGULA
‘JOHARI’ Unaweza kusema amesafiri au hayupo nchini kumbe amejichimbia katika kampuni yao ya RJ na mkurugenzi mwenza, Vincent Kigosi ‘Ray’ wanazitengeneza filamu zao kimyakimya. Mara nyingi unaweza kumuona Ray katika filamu au viwanja vya bata lakini Johari ni nadra sana.


YVONNE-CHERRY
NGATIKWA ‘MONALISA’

Mama yake ni mwigizaji na yeye pia, amefuata nyayo. Mara nyingi unaweza kusema hayupo nchini lakini ukweli ni kwamba anapiga mzigo katika levo za kimataifa na ana bidii ya kukua kila siku.

SABRINA RUPIA ‘CATHY’
Mama mwenye familia, anaigiza filamu zake huku akiwa mjasiriamali. Ukimtazama unaweza kusema haigizi lakini ukweli ni kwamba yupo ndani ya gemu kitambo toka Kundi la Sanaa la Mambo Hayo lililokuwa likirusha michezo yake runingani kabla halijafa.

WASTARA
Safari yake kwenye soko la filamu iligubikwa na changamoto nyingi, hakukata tamaa. Anapokuwa mzigoni huwa hapendi kujionesha, hufanya kwa vitendo zaidi. Kazi zake zinaonekana.
RIYAMA ALLY
Ni muigizaji mzuri, anajua kuuvaa uhusika. Linapokuja suala la kuonekanaonekana kwake huwa tofauti, huonekana mara chache sana katika matukio muhimu haswa ya kazi.

SALOME MISAYO ‘THEA’
Kabla hajaolewa, kidogo alikuwa akionekana japo si sana. Alipoolewa ndiyo kabisa. Zaidi utamuona pindi wanapokuwa ‘location’ au kwenye tukio muhimu linalohusishaa wasanii kwa jumla.
Idadi ya wasanii wanaofanya kazi zao bila mbwembwe ni kubwa lakini kutokana na uhaba wa nafasi hawa wanawawakilisha wenzao.