Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Dk. Harrison Mwakyembe.
Mawaziri wa uchukuzi wa nchi za Tanzania, Burundi na Rwanda wamekutana jijini Dar es Salaam jana kwa lengo la kutathmini mradi wa ujenzi wa reli utakounganisha nchi hizo tatu.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Dk. Harrison Mwakyembe alisema mradi huo unashirikisha nchi hizo tatu kwa lengo la kuboresha usafiri wa reli.

“Kwa sasa wataalamu wanaendelea kutathimini mradi huo ambao ulianza miaka miwili iliyopita, ila ripoti kamili kuhusiana na mradi huo inatarajiwa kutolewa na mtaalamu Machi mwaka huu,” alisema Dk. Mwakyembe.

Dk. Mwakyembe alisema kwa upande wa Tanzania, reli hiyo itajengwa kuanzia Dar es Salaam hadi Isaka kisha hadi Kigali/Keza- Gitega na kuishia Musongati nchini Burundi.


Alisema ujenzi wa reli hiyo utakapoanza, unatarajiwa kumalizika kabla ya 2016 kutokana na nchi ya Burundi wakati huo kuanza kuzalisha madini ya nickel ambayo yatakuwa yakitumia usafiri wa reli badala ya barabara.

Aidha, Dk. Mwakyembe alisema wakati wa ujenzi wa reli hiyo utakapoanza, kila nchi itabeba jukumu la kuigharamia isipokuwa mkopo ukiombwa utahusisha nchi zote tatu.
“Reli hii ikikamilika, itasaidia kuimarisha barabara zetu kwani mzigo mkubwa utakuwa hausafiri kwa barabara, hivyo kutumia reli kutasaidia kupunguza gharama za matengenezo ya mara kwa mara ya njia,” alisema.

Naye waziri wa uchukuzi wa Rwanda, Dk. Alexis Nzahabwanimana, makampuni zilizokuwa zikifanya upembuzi yakinifu wa mradi wa reli hiyo, zinatarajiwa kukamilisha ripoti mwishoni mwa Februari mwaka huu.

Dk. Nzahabwanimana alisema kampuni ya DB International ya Ujerumani ilianza upembuzi wake mwaka 2009 na kufuatia ile ya Burlington Northern Santa Fe, LLC (BNSF) ya Marekani (2010), hivyo kuwasilisha taarifa yake mwezi ujao.

“Pia naishukuru benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) pamoja na The United State Trade and Development Agency (USTDA) kwa kuweza kusaidia kufanikisha mchakato wa upembuzi huo wa ujenzi wa reli mpya. Bila mchango wao tusingefikia hapa,”    alisema Dk. Nzahabwanimana.

Akizungumza katika mkutano huo, waziri wa uchukuzi wa Burundi, Injinia Moise Bucumi alisema mradi wa ujenzi wa reli hiyo utakapokamilika utasaidia kukuza uchumi wa nchi zote tatu ambazo zitakuwa zikitumia reli hiyo.

“Tutapata wawekezaji wengi katika nchi zetu kwani usafiri utakuwapo wa kusaidia kusafirisha bidhaa toka katika bandari ya Dar es Salaam hadi Kigali na Burundi,” alisema Injinia Bucumi.

 

CHANZO: NIPASHE